HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 20, 2019

Kampeni ya 'Linda Ardhi ya Mwanamke' kuzinduliwa kesho, Tanzania yachaguliwa kuiendesha

Na Janeth Jovin

MWENYEKITI wa Kampeni ya 'Linda Ardhi ya Mwanamke', inayoratibiwa na asasi za kiraia 26,  Tike Mwambipile amesema kuwa Tanzania imechaguliwa kuendesha kampeni ya 'Linda ardhi ya mwanamke'  inayoratibiwa na asasi za kiraia 26, yenye lengo la kumsaidia  mwanamke  kuweza kumiliki ardhi yake mwenyewe.

Mwambipile amesema pia bado mila na desturi kandamizi ni masuala yanayosababisha wanawake wengi nchini kushindwa kumiliki ardhi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwambipile anasema mila na desturi kandamizi zimekuwa zikiwakwamisha wanawake wengi kupata ardhi ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Anasema anaamini kuwa uwepo wa kampeni hiyo ambayo  itazinduliwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na watoto Ummy Mwalimu, itawawezesha wanawake kumiliki ardhi na kufaidi mapato yanyokanayo na ardhi hiyo.

Mwambipile anasema lengo la kampeni hiyo ni kufunga ombwe lililopo kati ya sera au sheria na taratibu  za maisha ya kila siku ya jamii za watanzania ikiwemo kubadili fikra za wanajamii kutoka katika mila kandamizi zinazozuia mwanamke kumiliki ardhi.

"Unaweza kwenda kijijini ukamwambia mwanamke kuwa unauwezo wa kumiliki ardhi akakataa kabisa na hiyo inatokana na mila na desturi tulizonazo ambazo nyingi zinamkandamiza mwanamke, ila naamini elimu ikitolewa wanawake watatuelewa.

"Na ndio maana tumekuja na kampeni hii ambayo italenga pia kuongeza nguvu ya haki ya wanawake kumiliki ardhi, kutoa maamuzi kuhusu ardhi na kufaidi mapato yatokanayo na ardhi," anasema

Anasema anaamini kuwa matokeo ya kampeni hiyo ni zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wawe na uwezo wa kudai haki zao katika ardhi, kuboresha maisha ya kiuchumi, kuongeza na kuboresha upatikanaji wa ardhi kwa mwanamke.

Naye Mratibu wa Kampeni, Dk. Monica Mhoja anasema kampeni hiyo inafanywa kwa kushirikiana na Serikali hasa ngazi ya vijijini mahali ambapo wanawake wengi wananyanyasika.

No comments:

Post a Comment

Pages