HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 18, 2019

MARUFUKU AFISA UGANI KUSAFIRI NJE YA KITUO CHA KAZI KIPINDI CHA KILIMO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akifundisha matumizi sahihi kunyunyuzia dawa za kuua wadudu haribifu wa mazao jana kwa  wakazi Wilayani Igunga   wakati uzinduzi wa  msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Tabora.
 

Na Tiganya Vincent

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amesitisha kwa muda likizo za Maafisa Ugani na Maafisa Kilimo wa ngazi zote, huku akiwataka kutumia kipindi msimu wa kilimo kwenda kwa wakulima kwa ajili ya kutoa elimu na kuwasaidia kulima kilimo bora.

Mwanri alitoa kauli hiyo jana Wilayani Igunga wakati akizungumza na Wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo Pamba na Maafisa Ugani kutoka Halmashauri mbalimbali alipokuwa akizindua msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Tabora.
Alisema kimsingi likizo ni haki ya Mtumishi yoyote, lakini inapaswa kutoa athari shughuli za uzalishaji kwa wakulima ambao wanategemea maelekezo kutoka kwao kwa ajili ya uzalishaji wenye tija.

“Kipindi hiki mvua zimeanza kunyesha na tayari wakulima wameanza kulima …mnapaswa kwenda kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima mazao yote kwa kufuata kanuni za kilimo bora…kila zao ni lazima lilimwe kwa kuzingatia vipimo na liwe katika mstari ili kuongeza uzalishaji...ni marufuku kwa Afisa Ugani kusafiri nje ya Kituo chake kipindi hiki labda kwa dharura na kwa sababu ambayo iko nje ya uwezo wa binadamu” alisema.
 
Alisema wakulima wasiposaidiwa wataendelea kulima kilimo cha duni na cha kizamani ambacho wanatupa mbegu bila utaratibu na kuwa na uzalishaji wa kujikimu badala ya kuzalisha ziada ambayo itasaidia kujiendeleza na viwanda nchini kupata malighafi za kutosha.

Mwanri aliongeza Afisa Ugani wakati wa masika ni sawa na alivyo Mwalimu kipindi cha masomo naye hawezi kwenda likizo kipindi ambacho shule zinakuwa bado hazijafungwa.

Alisema mara baada ya shughuli za kilimo kumalizika , Maafisa hao wataruhusiwa kuendelea na likizo zao za mwaka na kuwataka Maafisa Utumishi kupanga Kalenda za likizo za watumishi hao kwa kuzingatia kalenda ya kilimo.

No comments:

Post a Comment

Pages