Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi (kushoto), Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Tanzania Bara, Twalib Njohole na Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Zanzibar, Asia Filfil Thani, wakifuatilia Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Hakimili za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (UPOV) nchini Uswis. (Na Mpiga Picha Maalum).
NA SULEIMAN MSUYA
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi
ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu nchini Tanzania (TOSCI), Dk. Patrick Ngwediagi amechaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Sheria (CAJ) ambayo ni Kamati Tendaji
ya Taasisi ya Kimataifa ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za
Mimea (UPOV).
Akizungumzia uteuzi huo
Dk. Ngwediagi alisema unatokana na mchango
wake kama mwakilishi wa Tanzania kwenye Baraza la UPOV na ushiriki makini wa
Tanzania katika shughuli na kazi mbali mbali za ulinzi wa hakimiliki.
Alitolea mfano usimamizi wa mashirikiano katika masuala ya hakimiliki
katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika
Mashariki ni sababu moja wapo ilisababisha kuchaguliwa.
Alisema Tanzania
imekuwa na mchango mkubwa katika masuala ya hakimiliki hivyo ni imani yake hiyo
imekuwa sababu ya kuchaguliwa na kuahidi kuwa ataitendekea haki nafasi hiyo.
“Hii ni taasisi
iliyoundwa na Serikali za nchi wanachama kusimamia na kuratibu taratibu za
utoaji na ulinzi wa hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu nashukuru
kupata nafasi hii nitahakikisha siiangushi nchini na Afrika kwa ujumla,”
alisema.
Alisema nafasi hiyo
ameipata baada ya kupendekezwa na kuungwa mkono na nchi kutoka mabara yote
kabla ya kuchaguliwa rasmi na Baraza Kuu la UPOV.
Dk.Ngwediagi alisema katika
kipindi cha miaka mitatu ya Uenyekiti wake, atahakikisha kuwa UPOV inafanya
maamuzi yanayoendeleza sekta ya kilimo kwa Tanzania, Afrika na kimataifa.
“Nitahakikisha Tanzania
na nchi zingine za Afrika zinanufaika na ujuzi na uzoefu mkubwa uliopo duniani
katika masuala ya utoaji wa hakimiliki kwa wagunduzi wabegu na katika sekta
nzima ya kilimo.
Tayari nimekwisha anza
kufanya majadiliano na baadhi ya nchi kama Uholanzi ambao wamepiga hatua kubwa
sana katika eneo hili pamoja na sekta nzima ya kilimo,” alisema.
Alisema majadiliano
hayo yanaonesha yatazaa matunda hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine
wataalam wetu watapata nafasi zaidi ya kujifunza jinsi wenzetu wanavyotumia
na walivyonufaika na uwepo wa hakimiliki
katika utafiti na ubunifu.
Aidha, alifafanua hakimili
inayotolewa kwa mgunduzi au mbunifu huwashawishi na kuwahamasisha wagunduzi watafiti
(breeders) kuendelea kufanya utafiti zaidi kwa umakini na ubunifu zaidi kwa
imani kuwa ubunifu wao hautatumiwa kinyume na matarajio bila kumshirikisha
mgunduzi.
Alisema katika kuhakikishiwa
ulinzi na heshima hiyo ndani na nje ya nchi, wanatoa mbegu bora zaidi
zinazohimili mazingira mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na hivyo
kuwasaidia wakulima kuongeza mavuno, tija na kipato.
Aidha alisema uwepo wa
mbegu zilizotafitiwa vyema na kwa ubunifu mkubwa huwezesha mbegu kupatikana kwa
wingi na kwa bei nafuu.
“Kwa ufupi hakimiliki
ni moja ya mazingira muhimu katika kuimarisha uwekezaji wa kilimo,” alisema.
No comments:
Post a Comment