Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu |
Na Suleiman Msuya
TAKRIBANI watu 200 wanaambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU) kila siku hapa nchini.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi
(TACAIDS) Dk. Leonard Maboko wakati wa Mkutano wa Makatibu wakuu wa
Sekta ya Afya na Ukimwi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) wanaokutana jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo wa kisekta ni mwendelezo wa mikutano ya mbalimbali ya watendaji na
viongozi wa nchi za SADC tangu Tanzania kuchukua kiti cha uenyekiti
kutoka Namibia.
Akizungumza
kwenye mkutano huo uliofunguliwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.Zainab Chaula, Dk. Maboko
alisema takribani watu 200 huambukizwa VVU kwa siku.
Alisema
takwimu zinaonesha watu 80 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi
24, huku kati ya hao vijana wanaopata maambukizi, watu 60 ni vijana wa
kike.
“Katika Siku moja
watu 200 wanaambukizwa VVU, 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24,
lakini changamoto zaidi ni kwa vijana wa kike, kwa sababu katika vijana
80 wanaopata maambukizi vijana wa kike ni 64,"alisema.
Alisema
Serikali inahakikisha inawawezesha wasichana walio katika mazingira
magumu kiuchumi kupata mahitaji yao ya muhimu na waweze kukaa shuleni
ili kujinga na janga hilo.
Dk. Maboko alisema mapambano dhidi ya maambukizi ya ukimwi yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima ili kuweza kuyakabili.
Alisema iwapo kila mwanajamii atakuwa mwalimu ni dhahiri maambukizi yatapungua kwa kiwango kikubwa.
"Sisi
kama nchi mwanachama SADC tunapaswa kushirikiana ili kupunguza
maambukizi haya kwani nguvu kazi kubwa inaathirika," alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Dk.Chaula mkutano huo utajikita kujadili mambo mbalimbali ya afya ikiwemo VVU ambayo ni tatizo pia.
Alisema
pia Serikali imejipanga kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini,
ikiwa ni moja kazi ya malengo ya nchi za SADC ifikapo mwaka 2030.
Katibu
mkuu huyo alisema watajadili jumla ya ajenda 13 kuhusu masuala ya Afya,
hususani HIV/AIDS, Malaria, TB na usambazaji wa dawa.
“Ajenda
yetu kubwa ya kwanza, ni kujadili namna ya kuutokomeza ugonjwa wa TB,
tunataka inapofika Mwaka 2030 nchi zote za SADC zisiwe na ugonjwa
huo,"alisema.
Dk. Chaula
alisema baadhi ya ajenda zingine zitazojadiliwa katika Mkutano huo, ni
masuala ya kutokomeza ugonjwa wa malaria katika nchi wanachama wa SADC.
Aidha,
Dkt. Chaula alisema kuwa, nchi ya Tanzania, kupitia Bohari kuu ya Dawa
nchini (MSD) imepewa heshima kubwa katika jukumu la kusambaza dawa,
vifaa na vifaa tiba katika nchi zilizo katika Jumuiya ya SADC.
“Nchi
yetu ya Tanzania imepewa heshima kubwa ya kusambaza dawa, vifaa na
vifaa tiba, kupitia MSD katika nchi za SADC”, alisema Dk. Chaula.
Chaula
alisema masuala ya Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Chanjo ni baadhi ya
ajenda zitazojadiliwa baina ya nchi wanachama wa Mkutano huo wa SADC,
ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha Sekta ya Afya.
No comments:
Post a Comment