Emmanuel Lyimo kutoka Shirika la Utunziaji wa Misitu Tanzania (TFCG)akitoa mada katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu habari za utunzaji wa misitu inayofanyika kwenye hoteli ya Oacis mjini Morogoro kwa siku mbili.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Utafiti uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) katika Wilaya 67 na Mikoa 22 Nchini umebaini upotevu wa misitu unachangiwa na kilimo kwa asilimia 89.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Utafiti uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) katika Wilaya 67 na Mikoa 22 Nchini umebaini upotevu wa misitu unachangiwa na kilimo kwa asilimia 89.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo wakati akitoa matokeo ya utafiti huo uliofanywa kwa miezi 6 katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS).
Katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika Mkoani Morogoro, zaidi ya waandishi 28 kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipewa matokeo ya utafiti huo pamoja na mafanikio ya mradi wa TTCS unaotekelezwa katika Wilaya ya Kilosa vijiji 20, Mvomero vijiji 5 na Morogoro vijiji 5.
Akizungumzia utafiti huo uliofanyika mwezi Juni hadi Novemba mwaka 2018, Lyimo amesema walilazimika kufanya utafiti ili kubaini ni sababu ipi kati ya kilimo na ukataji mkaa inayochangia upotevu wa misitu, ambapo walibaini kilimo ndio sababu kubwa.
"Utafiti umetuonyesha ukataji misitu kwa ajili ya kuandaa mashamba mapya unachangia upotevu wa misitu kwa asilimia 89, ukataji mkaa ni asilimia 35 na sababu nyingine niza mbao, ulimaji ndani ya misitu na makazi". amesema.
Lyimo amesema utafiti huo ulihusisha mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Morogoro, Singida, Tabora, Katavi, Rukwa, Kigoma, Mwanza, Mara, Simiyu na Geita.
Mkurugenzi huyo amesema utafiti huo ulishirikisha watu mbalimbali kama Maofisa mbalimbali, viongozi wa Serikali za vijiji na wananchi ambapo asilimia kubwa walibainisha kwamba mashamba mapya yanachangia upotevu wa misitu.
"Utafiti unaonyesha wananchi wanakata miti kuandaa mashamba, lakini awali inaonekana kama vile walikuwa wanaonekana kama walikuwa wanachoma mkaa" amesema.
Lyimo amesema kutokana na sintofahamu hiyo ya ni kipi kinachangia upotevu wa misitu wameamua kushirikisha waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo pamoja na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo mradi wa mkaa endelevu unatekelezwa ili kujionea namna Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) unavyochangia uhifadhi wa misitu kuwa endelevu.
Amesema wao kama shirika kwa sasa wanaamini ukataji mkaa unaozingatia utaratibu shirikishi na wenye kunufaisha wananchi hauna madhara katika misitu kama ilivyo kilimo hivyo wanaiomba Serikali kusisitiza USM kama njia ya kukabiliana na upotevu.
Naye Ofisa Kujengea Uwezo wa TFCG, Simon Lugazo amesema mradi wa TTCS katika Wilaya tatu za mwanzo umeweza kuchochea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na uhifadhi katika vijiji husika.
Lugazo amesema vijiji 20 vilivyo katika mradi vimepata huduma za kijamii kama ujenzi wa madarasa, zahanati, ofisi, maji huku baadhi ya wananchi wakinufaika kwa kujenga nyumba za kisasa, kusomesha watoto, kujiunga na vikundi vya hisa na kushiriki kilimo hifadhi.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TFCG, Bettie Luwuge amesema mafunzo hayo yataongeza chachu ya waandishi wa habari kuandika habari za mazingira na uhifadhi.
"Mazingira na uhifadhi ni vitu vinavyoenda kwa pamoja, ni imani yangu mtaieleza jamii ni namna gani ikitumia rasilimali misitu kwa mfumo endelevu itaweza kibadilisha maisha na kuleta usawa kijinsia" amesema.
Amesema TFCG, Mjumita na TaTEDA wataendelea kushirikiana na waandishi wa habari ili kuhakikisha dhana nzima ya usimamizi shirikishi inamfikia mwananchi.
No comments:
Post a Comment