HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 15, 2019

VIJIJI VYOTE VITAPELEKEWA UMEME-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum Arusha, Joyce Mukya, Bungeni jijini Dodoma, Novemba 13, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 
 

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema zoezi la usambazaji wa huduma ya nishati ya umeme linaloendelea kufanyika nchini hususan kwenye maeneo ya vijiji kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni endelevu.

”Mheshimiwa Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme ifikapo 2021. Kazi hiyo inaendelea vizuri kwa usimamizi wa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 14, 2019) katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza.
Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu vijiji ambavyo bado vitakuwa havijaunganishiwa umeme hadi 2021 ambao ni muda wa ukomo wa miradi ya REA.
Waziri Mkuu amesema hakuna kijiji kitakachokosa kuunganishiwa huduma hiyo na ili kuhakikisha inawafikia wananchi wote gharama za kuunganisha umeme vijijini zimepunguzwa na sasa ni sh 27,000 tu.
Amesema mbali na kupunguzwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme, pia Serikali imefuta gharama za bidhaa nyingine za kupeleka umeme kwenye maeneo yao ikiwemo nguzo na nyaya.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira kwenye sekta za afya, elimu na kilimo na hivi sasa inatarajia kutoa vibali 16, 000 vya ajira za walimu na kisha itatoa vya watumishi wa afya.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid  Shangazi, ambaye alihoji, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanapatikana watumishi wa kutosha kuwahudumia Watanzania.
Amesema mkakati wa kujenga miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali nchini unakwenda sambamba na kuajiri wataalamu watakao wahudumia wananchi katika maeneo husika.
”Serikali imeanza kutoa vibali vya ajira katika sekta hizi mbili za afya na elimu, hata kwenye kilimo. Mwaka jana tuliajiri watumishi 6,000 na sasa tuna kibari ambacho kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa upande wa sekondari na msingi.”

No comments:

Post a Comment

Pages