HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2019

Wanufaika wa TASAF walilia maofisa mifugo

Asha Shabani mnufaika wa mradi wa mbuzi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) anaomba kutembelewa na maofisa mifugo ili kufanya ufugaji wenye tija.
 

Na Irene Mark, Arusha

WANUFAIKA wa miradi ya mifugo inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wameiomba Serikali kuwaongeze ofisa mifugo ili wafuge kwa ufanisi.

Wanufaika hao wanatoka kwenye kata za Monduli Juu na Mfereji zenye vijiji sita vinavyomtegemea ofisa mifugo mmoja.

Kwa nyakati tofauti wanufaika hao waliozungumza na Jamvi la Habari, walisema wanafanya ufugaji kwa kudura za Mungu huku wakieleza namna mifugo yao inavyokufa kwa kukosa miongozo ya wataalam.

Magreth John mkazi wa kijiji cha Mbuyuni wilayani Monduli, alisema alikosa ushauri wa kitaalam na kusababisha Kuku wake saba na mbuzi mmoja kufariki.

"Tangia nimepewa huu mfugo bwana wanyama alipita safari moja tu na mbuzi aliumwa kizunguzungu akafa akaacha mtoto ndio huyu naendelea nae," alisema John.

Maria Laizer anasema bwana mifugo anapita mara moja moja sana hivyo ugonjwa ukiingia ni rahisi kuku na mifugo mingine kufa hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujikwamua na umaskini.

Mratibu wa TASAF Wilaya ya Monduli, Linetteh Chiduo alikiri kuwepo kwa uhaba wa maofisa mifugo hivyo kuiomba Serikali kupitia Wizara husika kupeleka maofisa mifugo wa kutosha wilayani humo.

"Hapa changamoto yetu kwenye utekelezaji wa miradi yetu ni uhaba wa maofisa mifugo, yupo mmoja anategemewa kwenye kata mbili nazo vijiji vyake vipo mbalimbali mno.

"Sasa analemewa wanavijiji wengi wanafanya ufugaji naona kabisa amezidiwa," alisema Chiduo na kutaja mifugo iliyotolewa na TASAF kwa ajili ya kuwapa wanufaika shughuli ya kuwapatia kipato kuwa ni kuku, kondoo na mbuzi.

Kwa mujibu wa Chiduo, walengwa wa TASAF wilayani Monduli wapo 5,863 kati ya 6,242 walioanza na mradi mwaka 2015.

Alitaja vijiji vilivyopata mbuzi kuwa ni Nafco, Oltukai, Lemoti, Jangwani na Mfereji wakati Kijiji kilichopata  kondoo 210 ni Emairete ambapo kaya zilizonugaika ni 168.

Alisema kuku 85 walipelekwa kwenye kijiji cha Jangwani na kaya 27 zilinufaika huku akibainisha kwamba zaidi vijiji vinne vilipata mradi wa Kuku wa asili.

No comments:

Post a Comment

Pages