HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 12, 2019

AFRIKA SI BARA LA GIZA NI LA NURU

 
Baba wa Uzao wa Kanisa Halisi la MUNGU BABA akiwahutubia waumini wa Kanisa hilo (hawapo pichani) hivi karibuni.
 Waumini wa Kanisa  Halisi la MUNGU BABA wakifuatilia ibada iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Uzao wa Kanisa hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam
 Makuhani wa Kanisa Halisi la MUNGU BABA wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa Bustani Mpya ya MUNGU BABA mkoani Kigoma hivi karibuni.
  Waumini wa Kanisa  Halisi la MUNGU BABA wakifuatilia ibada iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Uzao wa kanisa hilo hivi karibuni mkoani Kigoma.


NA Mwandishi Wetu

UMEWAHI kujiuliza nini maana ya Bara kijiografia? Bara ni sehemu kubwa ya dunia iliyochomoza juu ya bahari.
Kwa kawaida, bara hukaliwa na watu, milima, mimea na wanyama wakiwemo viumbe wengine,ingawa viumbe hai wengi zaidi wanaishi baharini.

Sehemu hii ya dunia, ndiyo inayojulikana kama Bara. Na  sehemu nyingine ya dunia ni ile iliyoko chini ya bahari.
Neno “Afrika” limetokana na lugha ya Kilatini ya Roma ya Kale. Waroma kwa jina hilo hawakumaanisha Bara lote, bali eneo katika Tunisia ya leo tu.

Ukija kwa bara lenyewe la Afrika, limezungukwa na bahari karibu pande zote. Kuna kiungo chembamba cha nchi kavu upande wa kaskazini mashariki na bara la Asia kwenye rasi ya Sinai.

Upande wa kaskazini iko Bahari ya Mediteranea, upande wa mashariki kuna Bahari Hindi pamoja na Bahari ya Shamu na upande wa magharibi iko Bahari Atlantiki na kuna kisiwa kikubwa cha Madagaska.

Bara la Afrika, kuna nchi huru 54 zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa ambapo nchi kubwa ya Afrika ni Algeria na nchi ndogo kwa Afrika Bara ni Gambia.
 
Mwaka 2010, idadi ya wakazi wa nchi zote za Afrika ilipita bilioni moja ambapo  idadi yao iliongezeka katika miaka 40 iliyopita, ikipiku zile za nchi za Ulaya na Amerika.

Mwaka 1950 walikuwepo Waafrika milioni 229 pekee, idadi iliongezeka kuwa milioni 630 mwaka 1990 na milioni 1200 mnamo 2014.

Licha ya Afrika kuwa na rasilimali za kutosha kama madini,mito,bahari pamoja na ardhi lakini ndilo Bara linaloonekana kuwa na watu masikini zaidi duniani kuliko mabara mengine.

Mbali ya hilo, pia kumekuwa na msemo kuwa Afrika ni Bara la Giza wakimaanisha kuwa licha ya kuwa na rasilimali za kutosha. Hata hivyo, wameshindwa kuondokana na hali ya umasikini.

Kwa upande wa Kanisa Halisi la MUNGU BABA lenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam  chini ya Baba wa Uzao wa MUNGU BABA, linathihirisha kuwa Afrika si Bara la Giza bali ni Bara lenye Nuru.

Kanisa hilo ambalo limekuwa likifanya mambo makubwa juu ya waumini wake na jamii inayowazunguka pamoja na  kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kumkomboa mwananchi juu ya  wimbi la umasiki limeweka wazi kupitia maandiko kuwa Afrika ni Bara lenye Nuru.

Kanisa hili linaloamini katika misingi mitatu ambayo ni AMANI, UPENDO na UZALISHAJI, limekuwa katika harakati za kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili kwa maana ya kutoishi maisha ya umasikini.

Linaamini, ili waumini wake waweze kuishi maisha ya kumsifu MUNGU BABA, limekuwa likihimiza kila mmoja kushiriki shughuli za uzalishaji mali ili kufuta Umasikini, Ufukara, Ombaomba na hali ya kuwa Tegemezi.

Akizungumzia kuhusu  Afrika ni Bara la nuru na sio giza,Baba wa Uzao wa Kanisa Halisi la MUNGU BABA,  anadokeza kwamba kuna maswali mawili makuu ambayo wamekutana nayo.
 
Swali la kwanza, ni kwa nini wanathubutu kusema Afrika ni nuru wakati yapo matatizo makubwa katika Bara hili yanayoonesha kuwa ni giza?

Baba wa Uzao, anasema, swali la pili ni kuwa, watafanyaje kuondoa hilo giza?

Anasema katika kujibu hayo maswali mawili, anatoa ufahamu wa mambo manne, kabla ya kuinua sauti kwa pamoja ya kuinua Bara la Afrika kuwa nuru.

Anasema moja kati ya mambo hayo manne ni pamoja na miduara mitatu iliyosumbua wote waliotumwa haipo tena milele (Ufunuo 12:1-9). Miduara hii mitatu ilikuwa ndicho kilele cha hila na ushetani.

Anasema jambo la pili ni utendaji wa nafsi ambao ulikuwa unaruhusu watu kuibiana Vipawa, Karama,Talanta na Viwekezo sasa umefika kwenye ukomo.

“Hiki ndicho kilikuwa kilele cha ubaya wa kila aina yaani, kuonea na kumzonga mwingine hatimaye kumwangamiza kwa sababu tu ya vitu vizuri alivyopewa na MUNGU BABA,”anasema Baba wa Uzao.

Baba wa Uzao anasema, jambo la tatu ni  utendaji wa moyo (ikiwa na maana ya kufika kwenye chanzo au chemchem ya Heri) umeanza rasmi ambapo katika kipengele kilichopita alisema ubaya umefika kwenye ukomo.

“Hapa heri sasa imeanza kwa maana ya kuishi unachosema, kuishi ya moyoni siyo ya mdomoni na Moyo wako kusomeka usoni kwako.

“Wengi hawajajua kwa nini Rais Dk. John Magufuli amefanikiwa ndani ya muda mfupi na kwa nini anapendwa na MUNGU BABA, ni kwa kuwa anaishi kile anachosema na huko ndiko kuishi Moyo.

“Na jambo la nne ni Sauti Mpya iliyoanzia Tanzania, Afrika, kwenda katika Mataifa mengine. Hiki ndicho kitu kikubwa ambacho kinasababisha sasa Afrika iwe nuru siyo giza.

UFAFANUZI KUHUSU MIDUARA MITATU
Akizungumzia juu ya miduara hiyo mitatu, Baba wa Uzao anasema  ilikuwa haijawahi kuguswa na Mtume au Nabii yeyote haipo tena ambapo mduara wa kwanza ni ule wa Ufunuo 12:1 wa pili ni ule wa Ufunuo 12:3-4; na wa tatu ni Mduara wa Ufunuo 12:7-9.

Anasema miduara hiyo haipo tena milele ambapo ilisumbua waliotumwa kuanzia Kerubi hadi Miaka 1000.

Baba wa Uzao anasema Kerubi katika Ezekieli 28:15(b) alidondoshwa na hii miduara mitatu, 2. Adamu wa Kwanza katika Mwanzo 3:1-6 alidondoshwa na hii miduara mitatu;
Anasema Musa katika Hesabu 20:9-10 aliangushwa na hii miduara mitatu ambapo Eliya Mtishibi katika 1 Wafalme 19:1-6 aliangushwa na hii miduara mitatu;

“Yesu katika Mathayo 21:37-39 na Mathayo 27:45-47 alinyang’anywa Urithi na hii miduara mitatu na hapa kwa Yesu najua waumini wengi wa madhehebu ya kikristo hawajawahi kuambiwa kweli, kuwa Urithi wao ulichukuliwa na dunia.”

“Eliya Adamu wa Pili katika Danieli 7:7 alisongwa na miduara hii mitatu kama waliomtangulia na Miaka 1000 naye pia katika Danieli 12:7-12 alisongwa na kuonewa na miduara hii mitatu.

“Miduara hii mitatu ambayo ni  Ufunuo, Nyoka na Vita ilikuwa inashirikiana kwa karibu kuhakikisha hakuna aliyetumwa anakatiza kwenda mbele,” anasema Baba wa Uzao.

UJUMBE
Akizungumzia kuhusu ujumbe wake kwa waafrika, Baba wa Uzao anasema matatizo yote ya Afrika, asilaumiwe yeyote, bali ni hiyo miduara mitatu ambayo ilikuwa inawaingia wale wote ambao wanaonekana  ni wakorofi.

“Giza, kwa maana ya umasikini na ubaya tunaoona katika Bara la Afrika, narudia kusema kuwa, ilikuwa ni hii miduara mitatu.

“Hata yule mwandishi wa Kitabu Kikubwa, aliyekiweka kwenye google, kuwa AFRIKA ni Bara la giza, aliingiwa na hii miduara mitatu, maana hizo ndizo nafsi zilizokuwa zinajua kuwa Afrika ni nuru, wakageuza kibao kuwa ni giza”anasema Baba wa Uzao

KWA NINI NASEMA MIDUARA HII MITATU HAIPO TENA?
Akizungumzia kuhusu kutokuwepo kwa miduara hiyo mitatu sasa, Baba wa Uzao anasema majira zilikuwa ni saba, kwa mujibu wa Mwanzo 1:1-31 na Mwanzo 2:1-4, yaani siku saba tu.
Katika Zaburi 90:4 na 2Petro 3:8 Kitabu kinasema kuwa siku moja ni sawa na Miaka 1000, na Miaka 1000 ni sawa na sikumoja tu,hivyo zile siku Saba ni sawa na Miaka 7000.
“Kila majira, kwa mujibu wa Ufunuo 20:6 ni Miaka 1000 peke yake! Hivyo, Waliotumwa wote saba wameshatimiza kazi zao kama ninavyoelezea hapa:
“Moja ni kwamba Majira ya Kerubi iliisha baada ya Adamu kuumbwa na kuanza kazi katika Mwanzo 2:15, Majira ya Adamu iliisha baada ya Musa kuanza kazi katika Kutoka 3:3-10, Majira ya Musa iliisha baada ya Eliya Mtishbi kuanza kazi katika 1Wafalme17:1.
“Nne ni kwamba Majira ya Eliya Mtishbi iliisha baada ya Yesu kuanza kazi katika Matendo 10:38,Majira ya Yesu iliisha baada ya Eliya Adamu wa Pili kuanza kazi katika Isaya 42:1,” anasema Baba wa Uzao.
Baba wa Uzao anasema majira ya Eliya Ad2 na majira ya Miaka1000 ndiyo iliyokuwa imefichwa kwa wengi kwani kwa mujibu wa Zekaria 4 na Ufunuo 11 majira ya Sita na ya Saba kuna Mizeituni Miwili ambayo inaonyesha kufanyakazi kwa pamoja.
Anaongeza, Theolojia ilificha jambo hili ingawa 1 Korinto 15:44-54 inaonyesha wazi kuwa yuko Adamu wa Pili ambaye ndiye Nabii wa Mwisho katika mfululizo wa vizazi vinne vya Ibrahimu.
Baba wa Uzao anafafanua kuwa Yesu pia katika Mathayo 17:10-13 aliweka wazi kuwa yeye siyo Nabii wa Mwisho, bali atakuja Eliya ili atengeneze yote.
Majira ya Sita na ya Saba ambayo kitovu chake ni Tanzania imeishaje?

Akifafanua kuhusu hali hiyo, anasema katika Mathayo 24:22, Yesu alisema Miaka 1000 itafupishwa, maana bila kufupishwa hakuna ambaye angeokoka.

“Kanuni ya kufupisha Miaka hiyo ni kuchukua miaka ambayo Musa alifanyakazi, kwa mjibu wa Luka 13:6-9, yaani Miaka 3 1 / 2 (ingawa theolojia inatambua miaka 40); kujumlisha muda ambao Eliya Mtishibi alifanyakazi Miaka 3 1 / 2; kujumlisha muda ambao Yesu alifanyakazi Miaka 3 1 / 2; na kujumlisha muda ambao Eliya Adamu wa Pili alifanyakazi Miaka 3 1 / 2.

“Jumla unapata Miaka 14. Ukichukua Miaka hiyo ambayo inatokana na kazi zilizofanyika katika vizazi vine vya Ibrahimu, kujumlisha na Mwaka 2003 ambapo Sauti ya Sita ilisikika Kigoma Tanzania, inakufikisha Mwaka 2017.

“Ibrahimu katika Mwanzo 15:16 aliambiwa na MUNGU BABA kuwa ikifika Mwisho wa vizazi vinne; ndipo utakuwa ukomo wa yeye kuwa Baba wa Mataifa yote,”anasema Baba wa Uzao.

Baba wa Uzao anabainisha kuwa, vizazi vyote vinne vimeshaisha kimahesabu na Majira zote Saba zimeshaisha kimahesabu tangu 2017.

“Katika 1 Yohana 5:8 kuna Nafsi Tatu Kuu zinazojulikana za MUNGU: Baba, Mwana na Roho.
“Katika Mwanzo 1:2, Roho alishakuja na Katika Mathayo 2:1 na Luka 2:21 Mwana naye alishakuja.

“Baba ndiye alikuwa amebaki. Baba alipokuja Mwaka 2017 niliwatangazia. Ametenda kazi kwa Miaka Miwili sasa na vitabu nimewaandikia,”anasema Baba wa Uzao.
Hata hivyo, Baba wa Uzao anasema kuwa kwa mujibu wa Danieli 12:7-12, hakuna Nabii wala Mtume ambaye angekatiza.

“Aliyeweza giza ni MUNGU BABA Mwenyewe siyo mwingine yeyote (1Korintho 15:28).

Nguzo kubwa ya hiyo miduara mitatu ilikuwa ni giza na hilo giza lilitanda AFRIKA ili tusijue BARAKA kubwa tuliyonayo.
“Baada ya hiyo Miaka miwili ya Utendaji wa Nafsi ya Baba, sasa Shamba ni Jipya kabisa, siyo tena lile la Mathayo 21:33-40 lililoharibiwa.

“Kwa kuwa hiyo miduara mitatu haipo, sasa giza katika Bara la Afrika haliwezi kuwepo tena. Maana yuko MUNGU BABA Mwenyewe ndani ya moyo wa kila anayempenda,” anasema Baba wa Uzao.

Hata hivyo, Baba wa Uzao anafafanua kuwa tofauti kubwa iliyopo sasa, kulinganisha na Majira au Vizazi Vilivyopita, MUNGU BABA sasa amebebwa na kila mmoja anayempenda, siyo mmoja tu anayesimama mbele ya wengine.

MIDUARA MITATU KUFUTIKA MAANA YAKE NI UKOMO WA UTENDAJI WA NAFSI.

Akizungumzia kuhusu hilo, Baba wa Uzao anaeleza kuwa katika majira zote saba, hali halisi ya maisha ilikuwa ni hii:
“Kila aliyekuwa anaachiliwa kutoka kwenye vitanga vya mikono ya MUNGU BABA (Isaya 49:16), alikuja akiwa tajiri, ila alipoingia tumboni mwa mama yake, alinyang’anywa ‘File’ lake saa hiyo hiyo!Hilo “file” ndilo lilikuwa na kila kitu kizuri: Vipawa;Karama; Viwekezo; na Talanta.

“Hiyo miduara mitatu ndiyo ilikuwa inafanya kazi hiyo ya kuteka nyara vitu vizuri ulivyokuja navyo, maana waliitwa: Ishara ya I; Ishara ya II; na Ishara ya III Mbinguni”anasema Baba wa Uzao.

Baba wa Uzao anasema, ndiyo maana katika Yeremia 1:5 MUNGU BABA anasema: “Kabla sijakuumba nilikujua, na kabla hujatoka tumboni kwa mama yako nilikutakasa.”
“Maana anajua vile vitu ambavyo alikuachilia ukiwa navyo walikunyang’anya na watu wengi waliamua kuabudu hii miduara mitatu baada ya kuona mambo hayaendi,”anasema Baba wa Uzao.

Baba wa Uzao anasema haya ya kunyang’anywa kila kitu, yalifanyikia kwenye nafsi, maana thamani iko kwenye nafsi na tatizo la nafsi haitunzi, ila inashika tu.

Anasema wale waliokaa Berlin na kugawanya Afrika walivuta nafsi ya Afrika kwenye Beseni na kuanza kuligawanya Bara la Afrika wakiambiana kuwa,‘Wewe chukua hiki; wewe chukua hiki; na wewe chukua hiki’.

“Walipomaliza kwenye Nafsi, ndipo wakaja kwenye uhalisia kutimiza walichofanyia kwenye nafsi na huo ndio uliokuwa Utendaji wa Nafsi.

“Mtu yeyote alikuwa ana uwezo wa kwenda kwa mganga na kupeleka jina lako na kusema nataka unipe vipawa, karama, talanta na viwekezo vya fulani.

“Mganga naye anachukua Beseni la maji mbele yako anaita nafsi yako, sura yako ikionekana pale kila kitu kinachukuliwa. Ndivyo walivyotia giza katika Bara la Afrika”anasema Baba wa Uzao.

 Anasema, sasa MUNGU BABA aliyetuumba sote amekuja kukomesha huo Utendaji milele. Haitatokea tena maana sasa ni Majira ya Utendaji wa Moyo, siyo Nafsi.

“Katika Majira Saba, mambo ya kulia yaliwekwa kushoto na yale ya kushoto yaliwekwa kulia, wenyewe wanaita “Cross–multiplication.” Sasa kila kitu kimerejea mahali pake milele.
“Kila mmoja amerudi kwenye Kusudi, Afrika nayo imerejea kwenye kusudi la kuwa nuru”anasema Baba wa Uzao

UKOMO WA UTENDAJI WA NAFSI MAANA YAKE MWANZO WA UTENDAJI WA MOYO:
Akifafanuwa kuhusu hilo, Baba wa Uzao anasema wengi walikuwa wakisoma Yeremia 50:20.

Lakini, walikuwa hawafahamu kuwa itatimia kwa jinsi ipi? Maana imeandikwa kuwa, majira inakuja na watatafuta uovu ndani ya jamii wala hawatauona.

Anasema hawakujua kuwa itatimia wakiwa wanaona kwa macho ambapo wakisema utendaji wa moyo,Maana yake nini hasa? utendaji wa moyo badala ya utendaji wa nafsi uliozoeleka, ni uumbaji mpya.

“Katikati ya nafsi na moyo ndipo kuna Korongo ambalo limejaa giza na MUNGU BABA aliyekuja juu ya nchi anakaa kwenye Moyo siyo kwenye nafsi.

“Jambo hili halikuwahi kutokea majira yoyote, la MUNGU BABA sasa kuishi ndani ya Moyo wa kila mmoja na sasa limetokea na limeanzia Tanzania Afrika  na hiyo ndiyo nuru.

“Ninachosema ni kuwa, kila mmoja ninapoendelea kuongea malaika wako wanamfanyia “operation” ili aanze kuishi maisha yafuatayo kama kuishi unachosema, kuishi ya moyoni, na hakuna tena na sikiliza maneno yangu lakini msiangalie matendo yangu.”

Baba wa Uzao anasema kuwa hilo ndilo Shamba Jipya na ndani yake kuna Bustani Mpya ambapo kuanzia sasa, kila mmoja, Moyo wako utasomeka kwenye uso wako.

KATIKA SHAMBA JIPYA NA BUSTANI MPYA NDIKO KUNA SAUTI MPYA
Akitoa ufafanuzi juu ya hilo, Baba wa Uzao anasema zile majira saba zilizoisha zilitokana na Sauti Kuu Saba za  MUNGU BABA ambazo, aliachilia kwa wale saba waliotumwa.

Anasema Sauti zote Saba zilitekwa nyara na ile miduara mtatu ambayo ilikuwa ni Ishara ya kwanza hadi ya tatu mbinguni.

Anasema, kila kilichokuwa kimebebwa na hizo Sauti Saba, kilichukuliwa na kutengeneza maendeleo ambayo tunayaona Ulaya, Amerika, Asia, Australia, New Zealand na Mataifa machache ya Afrika.

Anasema,  sasa majira na nyakati za sauti hizo saba haipo tena, bali tuna Sauti Mpya kabisa iliyosikika Afrika sehemu ya Kigoma Tanzania Lango la 26 Thebeti, 1 au 26 Mei, 2019.
“Kwa vyovyote vile Sauti hiyo ina Mamlaka ya kufuta giza la kila aina ambalo lilikuwa limewekwa katika Bara zima la Afrika.

“Ndiyo maana utasikia wakisema “hii ni Sauti ya Ujerumani kutoka dutch velle! Nikwa sababu, kiroho, makao yao makuu bado ilikuwa ni Kigoma,ambayo ni sehemu ya Afrika. Hapo ndipo hiyo Sauti Mpya ilisikika.

“Na wao walikuwa wanajua hilo ndiyo maana wakati wa Germany East Afrika waliweka makao yao makuu pale na kwa ufahamu huu sasa una uwezo wa kusimamisha nuru kutokea Afrika kwenda kote,”anasema Baba wa Uzao.

SASA TUNAINUA JUU NURU HII

Baba wa Uzao anasema, Mamlaka ya Uchumi wa Afrika, Lango la Afrika kurithishwa na MUNGU BABA, Afrika kukimbiliwa na mema tu, burudiko na kustareheshwa, Maachilio ya Afrika kutoka kwa MUNGU BABA,Afrika kuwa jibu la Mataifa;

Baba wa Uzao anasema Afrika kuwa nuru ya mataifa, Afrika kuwa Chanzo cha Baba, Afrika kuwa Kimbilio la Mataifa,Moja ya Afrika Halisi, yaani Lugha Moja; na Semi Moja, Afrika Chanzo cha Amani,Afrika Chanzo cha Uhai,Thamani ya Kazi za Afrika,Uhai na Ubora wa Kazi za Afrika;

Ufanisi, Ubunifu na Uvumbuzi wa Afrika,Viwanda vya Afrika,Umahili wa Afrika katika Mema tu, Uzalendo wa Mwafrika katika kuhakikisha Haki imesimama,Akili na Haki ya Mwafrika,Mwafrika kuwa Barabara ya Mema,Kweli ya Afrika,Uhuru wa Afrika,Amani ya Afrika,Utulivu wa Afrika;
Anasema Usalama wa Urithi wa Afrika (yaani Urithi wa Afrika kutonyang’anywa, kutoibiwa na kutopokonywa), Kuondolewa kwa Kongwa la Afrika, Sura Halisi ya Afrika;

“Tabia Halisi ya Afrika; Sifa Njema ya Afrika, Haki ya Afrika; Kuondolewa kwa sikio la kufa lililowekwa Afrika yaani kutofundishika “Uaminifu wa Mwafrika na  Ukarimu wa Mwafrika na Utoshelevu wa Mwafrika, na kujitegemea,Kuondolewa kwa Ngome za Ukooni na Ukoloni mambo leo Afrika,Kuondolewa kwa Alama za Kumbukumbu mbaya ya utumwa wa Mwafrika kupitia Mitaala Makumbusho na akili ya Mwafrika.

“Kuondolewa kwa Kidonda cha Mwafrika, maumivu na mateso ya Mwafrika, Kuondolewa kwa makovu na majeraha ya Mwafrika,Kuondolewa kwa Mwafrika kuwa mtumwa kwenye Nchi na Bara lake mwenyewe,”anasema Baba wa Uzao.

Anasema haki ya utajiri wa Mwafrika, Mfumo Baba unaoongoza Mataifa kutokea Afrika, Chanzo cha Lugha Baba Afrika, Utendaji wa Moyo wa Mafrika, Huduma ya Nuru inayotoka Afrika, Moyo unaotunza maoangezeko ndani ya Afrika, Chanzo cha Bustani Mpya Afrika, Utukufu na Heshima ya Afrika.

Anasema, Afrika Ikulu ya Mema, Afrika Hifadhi ya Mema, Afrika Chanzo cha mema, Macho, Kioo, na Sikio la Afrika, Uumbaji na Uhalisia wa Afrika, Nguvukazi ya Afrika, Uaminifu wa Vijana katika kukubali kutumika na MUNGU BABA Afrika na Wafalme kuleta Utajiri Afrika kama ilivyoandikwa katika Isaya 60 yote.

No comments:

Post a Comment

Pages