Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, akipokelewa na Ofisa
Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Jsoeph Witts, alipowasili katika
Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni kwa mikoa ya
Shinyanga, Geita, Kigoma na Tabora lililoandaliwa na benki hiyo mjini
Shinyanga. (Na Mpiga Wetu).
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Innocent
Bashungwa amewataka wakandarasi kutumia benki kuchukua mikopo ili kuwawezesha
kukamilisha miradi yao kwa wakati na kuacha kutegemea malipo ya awali ya mradi
husika ambazo zimekuwa zikichelewa na kufanya miradi kutokamilika kwa wakati.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza
katika kongamano lililoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wakandarasi
,wazabuni na wafanyabishara wa mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora na
Kigoma.
Kongamano hilo lililenga kuwapatia
washiriki hao elimu juu ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazozichukua
kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Bashungwa amesema wakandarasi ni
sekta muhimu sana katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini
hivyo wanapaswa kuboresha utendaji kazi wao kwa kuchukua mikopo toka
taasisi za fedha na mabenki.
Ameongeza kuwa, changamoto kubwa
inayowakabili wakandarasi wengi ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendesha
miradi mbalimbali ambapo changamoto hiyo huchangia kutomalizika kwa miradi kwa
wakati.
“Benki ya CRDB imewaletea fursa
mlangoni, itumieni vilivyo, changamkieni fursa hizo
ili muweze kukuza biashara zenu na kupata faida zaidi, kuongeza ajira kwa
vijana wetu na hatimaye kulipa kodi stahiki za serikali.
“Ni
matarajio yangu kuwa, baada ya kongamano hili tutaona utofauti kubwa kutoka kwa
wakandarasi na halmashauri ambao wamekuwa wakipitia changamoto katika
kukamilisha miradi yao, kutokana na suala la mapato na ukwasi” alisema
Bashungwa.
Bashungwa aliipongeza
Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali
katika ujenzi wa miondombinu mbalimbali ambayo itasadia kuchochea ukuaji wa
uchumi.
“Benki ya CRDB
inafadhili miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika jitihda zake za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na
wanatambua na kuthamini ushikiri wa benki hiyo
katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile Mradi wa Ujenzi wa Reli ya
Kisasa (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji katika Bonde la Mto Rufiji (Nyerere Hydro
Power Project) na ule wa kusambaza nishati ya umeme vijijini (REA).
“Kipekee
kabisa niwapongeze tena Benki ya CRDB kwa utayari wenu, ambao mmekuwa
mkiuonesha katika kuisaidia Serikali, hususani katika utekelezaji wa miradii
mikubwa ya kimkakati,” alisema Bashungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ya Kanda Ziwa,Aggrey Mwanri
aliwahamasisha wakandarasi na wazabuni wa miradi ya maendeleo katika
mikoa ya kanda hiyo ya magharibi kuchangamia fursa zinazotolewa na Benki ya
CRDB, ili kwa kushirikiana na serikali waweze kufikia lengo la kuimarisha
miundombinu nchini.
Awali,
Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB Dk. Joseph Witts amesema kongamano hili
ni fursa pekee ya kuwakutanisha wakandarasi, wazabuni na wafanyabisahra
ili kuwajengea uwezo na kuwajulisha fursa mbalimbali za kifedha zilizomo
ndani ya benki ya CRDB, na namna ya kuzitumia fursa hizo ili kukuza miradi na
biashara zao.
“Tuna
bidhaa nyingi mahususi kwa ajili ya kundi hili la wateja ikiwamo Purchase Order
Financing, Contract financing, and Invoice Discounting ambazo hazihitaji
dhamana yoyote kutoka kwa Mkandarasi au mzabuni pindi anapotaka kukopa.
“Zaidi ya
hilo, Benki pia hutoa mikopo kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi, magari,
mashine, Mabasi na huduma nyingine kama vile dhamana ya malipo ya awali
(Advance Payment Guarantee), dhamana ya Utekelezaji wa Miradi (Performance
Guarantee), Barua za Mikopo (Letters of Credit), Huduma za Bima na pia tunatoa
mikopo ya muda mfupi kama mitaji ya kufanyia kazi” alisema Dk. Witts.
Akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi hao,Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya ukandarasi ya Junior Construction Ltd na Mbunge wa Jimbo la Kishapu
Suleiman Nchambi aliipongeza Benki ya CRDB kwa hatua hiyo ya kuwakutanisha
wadau wa sekta ya ujenzi nchini huku wakieleza fursa zinazotolewa na Benki ya
CRDB zitakwenda kuleta sura mpya katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu
nchini.
No comments:
Post a Comment