HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 04, 2019

Chanzo cha ukosefu wa ajira kwa vijana chatajwa

Mkurugenzi Mtafiti Mkakati kutoka REPOA, Dk. Jamal Msami, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

 
Na Janeth Jovin

UTAFITI wa mwaka 2018/19 wa ukosefu wa ajira kwa vijana nchini na mchango wa vyuo vya ufundi stadi katika utoaji wa ajira, umebaini kuwa vijana wengi nchini wanashindwa kupata ajira kwa sababu elimu wanayopatiwa wakiwa vyuoni  haikidhi mahitaji ya soko la ajira mitaani.

Aidha utafiti huo ambao umetolewa na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (REPOA), umebaini pia wanafunzi wengi wanaojiunga na vyuo vya ufundi stadi wanakuwa na elimu duni hivyo kushindwa kufuatilia ipasavyo mafunzo yanayotolewa hali inayosababisha kutokidhi vigezo vya kuingia katika ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jana wakati wa majadiliano ya vijana kuhusiana na utafiti huo,  Mkurugenzi wa utafiti, REPOA Lucas Katera anasema vitendea kazi na miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi navyo ni moja ya vikwazo kwa wahitimu kushindwa kupata ajira.

Anasema pia wamebaini uwepo wa idadi kubwa ya walimu chuoni lakini wanafunzi wanaofundisha ni wachache  hivyo mwalimu kukosa fursa na mudi ya  kufanya kazi hivyo kusababisha kutowafundisha  vitu kwa vitendo badala yake anaishia nadharia tu.

"Vijana wengi wanaomaliza wakifika katika soko la ajira wanaonekana awahitajiki hii inasababishwa na sababu hizo nilizozisema, lakini pia  mfumo wa fedha hautoshelezi kuwapatia hao wahitimu mtaji wa kufanya biashara wanapokuwa wamemaliza chuo, mfano anaemaliza chuo kama mkulima anahitaji hela ili anunue trekta, sasa mfumo huo  wa fedha unajitahidi lakini haukidhi haja ya matarajio ya mtu," alisema.

Anasema kitu kinachopaswa kufanyika ili kuondokana na changamoto hizo ni kuboresha elimu ya msingi hadi Sekondari ili iweze kukidhi mahitaji ya kuwafanya wanafunzi wanaoingia katika elimu ya ufundi stadi waweze kufatilia masomo yao vizuri.

Naye Mkurugenzi Mtafiti Mkakati kutoka REPOA, Dk. Jamal Msami anasema utafiti huo umefanyika katika jumla ya halmashauri 25, pamoja na mambo hayo  pia imeonesha wanafunzi wengi katika vyuo hasa vya ufundi ni wanaume na hiyo inatoka na uwepo wa kozi nyingi wanazozimudu.

"Ni muhimu sana kufanya tathimini ya kina ili tuweze kuachana na mfumo inayotulazimisha kwenda katika kundi fulani tu," anasema.

No comments:

Post a Comment

Pages