Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango (Mb) akizungumza na washiriki wa Kongamano la Wanamipango ambapo
alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, Jijini Dodoma. Waziri Mpango amewataka
washiriki kuja na mipango ya kuibua fursa ambazo hazijaguswa ili kuweza kuinua
uchumi wa nchi.
Mgeni rasmi wa Kongamano la
Wanamipango Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa
kongamano hilo lililokutanisha wataalamu wa masuala ya mipango kutoka Wizara,
Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya
Serikali za Mitaa pamoja na Sekta Binafsi Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini
Dodoma. (Picha na Wizara ya Fedha na Mipango,
Dodoma).
Na Farida
Ramadhani na Saidina Msangi,
WFM, DODOMA
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango
amewaagiza wataalamu wa mipango nchini kutoa mapendekezo ya kibunifu ambayo
yataiwezesha nchi kunufaika na utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta
binafsi (PPP).
Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Kongamano la Wanamipango
kwa mwaka 2019 lililofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango,
jijini Dodoma.
Alisema kuwa bado kunachangamoto ya utekelezaji wa PPP
nchini na kuwataka wataalamu hao kujadili ili kuona wapi nchi imekosea na kutoa
suluhu ya namna ya kutatua changamoto hizo.
“Lakini PPP
niliyoona imefanikiwa sana ni kwenye sekta za kijamii, najua tumefanya vizuri
kwenye huduma za afya na elimu, lakini kweye miradi ya miundombinu bado”,
alibainisha.
Aidha, Dkt. Mpango aliwagiza wataalamu hao kujadili
namna bora ya kutanua wigo wa kukusanya kodi ili kuiwezesha nchi kuweza
kujiendesha pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema katika suala la kodi, ukusanyaji kodi bado
kuna shida kwani hata idadi ya walipakodi ni ndogo ukilinganisha na idadi ya
wananchi.
Aliwataka wataalam hao kuhakikisha wanasimamia
ukusanyaji mapato ya Serikali na kuhakikisha yanatumika vema ili kuweza kukuza
uchumi wa nchi.
Aliseme ni vema wataalam hao wakatambua kuwa katika
harakati za kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ni wazi baadhi ya vyanzo vya
ugharamiaji wa miradi vitapungua hivyo ni lazima nchi iweke mipango madhubuti
ya kutafuta rasimali kutoka katika vyanzo mbadala vya mapato za kuweza
kugharamia miradi hiyo.
Waziri Mpango alisema kwa kuwa Kongamano hilo
linalenga kujadili namna ya kugharamia maendeleo, ni vema wataalamu hao
wakajadili na kujatoa muongozo wa namna Tanzania itakavyoweza kuvutia
wawekezaji binafsi kwa wingi.
“Ni matarajio ya Serikali kongamano hili litajadili wawekezaji
ambao watafanya uwekezaji utakao inufaisha nchi na wao wenyewe, yaani uwekezaji
huu uwe ni win-win”, alifafanua.
Aidha, Dkt. Mpango aliwaagiza wataalam hao kujadili
namna majukumu ya benki za ndani katika kugharamia miradi ya maendeleo ili
kuona namna ya kuzishirikisha katika miradi hiyo.
Naye Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.
Lorah Madete alisema kuwa kupitia kongamano hilo washiriki watapata fursa ya
kujadili mawasilisho yatakayoendana na dhima ya kongamano ikiwemo Vyanzo bunifu
vya ugharamiaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, Sera, Sheri ana Kanuni.
Kongamano hilo la siku mbili limekutanisha wataalamu
wanaohusika na masuala ya mipango kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala
za Serikali, Taasisi, Sekretariaeti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na
Sekta Binafsi.
No comments:
Post a Comment