Vikosi vya Yanga SC na KMC vikiingia dimbani mchezo wa Ligi Tanzania Bara (VPL) ambapo mtanange huo umemalizika kwa sare ya bao 1-1. (Picha na Yanga SC)
Na John Marwa
KIPORO kimegoma kulika, unaweza kusema hivyo baada ya Mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Yanga SC, kulazimishwa sare ya bao 1-1 na vijana wa 'Kino Boys' KMC mchezo wa VPL uliolindima leo Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga waliingia kwenye kandanda hilo wakiwa na mzuka wa kushinda mechi tatu mtawalia tangu iwe chini ya Kocha wa muda Charles Mkwasa 'Master' akipokea kijiti cha Mcongo Mwinyi Zahera aliyetupiwa virago.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kucheza soka la kuvutia huku zikitengeneza nafasi ambazo hazikutumika vyema.
Mshambuliaji wa Yanga SC David Molinga akiingia Uwanjani mchezo wa VPL Yanga walipoialika KMC Taifa.
Yanga walikuwa wa kwanza kuandikisha bao la kuongoza dakika ya 73 kupitia kwa Mkongwe Mrisho Ngasa, aliyeambaa na mpira huku mabeki wa KMC wakishindwa kumdhibiti kutokana na kasi yake na kuweza kufunga bao.
Wakati Yanga wakiamini wanaibuka na pointi tatu muhimu mambo yalibadilika dakika za mwisho baada ya kushindwa kuhimili mashambulizi ya safu ya ushambuliaji ya KMC na kusababisha madhabi yaliyopelekea Mwamuzi kuwazawadia KMC mkwaju wa penati, uliowekwa kimiani na Abdul Hillary dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo Yanga wamefikisha pointi 17 za michezo nane nafasi ya nane kwenye msimamo wa VPL wakishinda mechi tano sare mbili na kupoteza mmoja, huku KMC wakiwa nafasi ya 17 pointi tisa michezo 11.
Kikosi cha Yanga SC kilichomenya na KMC hivi leo, kandanda la VPL
Mchezo mwingine wa VPL uliolindima leo ni kati ya Biashara United ya Mara waliowaalika Ndanda FC na Ndanda kukubali kichapo cha bao 1-0 katika Uwanja wa Karume mjini Musoma, Bao la Bright Obina dakika ya 22 likiipatia Biashara pointi tatu mujarabu.
Michezo hiyo ya leo inaipeleka VPL mapumzikoni hadi januari 2020 kupisha mashindano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inayotarajia kuanza hivi karibuni nchini Uganda.
No comments:
Post a Comment