MAANDALIZI ya Mashindano ya Taifa ya Riadha mwaka 2019
yanayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza katika Chuo cha Elimu ya Taifa Butimba,
yanaendelea vema.
Mashindano hayo ambayo mwaka huu yatajulikana kama Ngorongoro
Crater National Athletics Championship 2019 yatafanyika tarehe 28 na 29 Desemba
yakishirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), likitambua michango na
uwezeshaji wa wadau mbalimbali katika sekta ya michezo hususan Riadha, pia
likitambua wajibu wa michezo hususan Riadha katika kuchangia maendeleo ya Taifa
ikiwamo kuitangaza nchi na vivutio vyake, limeamua mashindano ya mwaka huu
yajulikane kama ‘Mashindano ya Riadha ya Taifa ya Ngorongoro Crater 2019’ hasa
tukiheshimu ushirikiano na sapoti kubwa iliyofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya
Bonde la Ngorongoro (NCCA), katika kalenda ya RT 2019 inayokwenda kumalizika
mwaka huu.
Katika kalenda hii inayokwenda kumalizika, NCCA imetoa
mchango kubwa katika kufanikisha Mashindano ya Nyika ya Taifa 2019
yaliyofanyika mjini Moshi Kilimanjaro, ushiriki wa Tanzania katika mashindano
ya Nyika ya Dunia huko Aarhus nchini Denmark, Mashindano ya Wazi ya Taifa 2018
yaliyofanyika jijini Arusha na matukio mengine mbalimbali. RT tunawashukuru na
kuwaomba wazidi kuendeleza ushirikiano na RT pia tunawakaribisha wadau wengine
wenye mapenzi mema na maendeleo ya Taifa la Tanzania hususan katika sekta ya
michezo, tutawapa ushirikiano wa kutosha.
Mikoa inatakiwa kuendelea kuwasiliana na Ofisi ya RT kwa
maelekezo zaidi endapo kuna jambo wanahitaji
ufafanuzi na timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza Desemba 27 mwaka
huu.
Maelezo zaidi kuhusu michezo itakayochezwa, idadi ya washiriki
kwa kila mkoa, imetumwa kwa makatibu wa mikoa yote na tunaomba izingatiwe.
Mashindano ya Taifa ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee hasa
ikizingatiwa hivi sasa tunakwenda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa
hususan Mashindano ya Dunia U 20 Nairobi Kenya, Olimpiki Tokyo 2020 na
mengineyo, hivyo yatatoa nafasi kwa vipaji vipya kuonekana na pia wachezaji
kuonyesha viwango vyao walivyo navyo hivi sasa, hivyo Shirikisho kuwa na
‘Active Data Base’ ya viwango vya wachezaji mbalimbali nchini na kuirahisishia
Kamati ya Ufundi katika utendaji wake kuelekea matukio hayo ya kimataifa.
Hivyo
tunasisitiza mikoa iwape nafasi wachezaji wao kuonyesha viwango vyao walivyo
navyo hivi sasa.
UCHAGUZI KAMISHENI YA WANARIADHA
Katika utekelezaji wa matakwa ya Kikatiba, Kamisheni ya
Wanariadha inapaswa kufanya uchaguzi wake mkuu sambamba na mashindano ya Taifa
mwaka huu baada ya kipindi chao cha uongozi kupita.
Hivyo Kamisheni ya Wanariadha itafanya uchaguzi wake Desemba
29 jijini Mwanza mara baada ya kumalizika mashindano ya Taifa. Hivyo Wachezaji
‘Active’ wenye nia ya kugombea watume maombi yao RT.
Nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Wajumbe wawili
wanaume na Wajumbe wawili wanawake.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO –RT
DESEMBA 24, 2019
No comments:
Post a Comment