HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 29, 2019

TABORA MARUFUKU KUCHEZA POOL ASUBUHI

Na Tiganya Vincent

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amepiga marufuku watu wazima na vijana kucheza michezo mbalimbali ikiwemo ‘pool’, bao na karata nyakati za asubuhi ili waweze  kutumia muda huo kwenye shughuli za kilimo na uzalishaji mali.

Hatua hiyo itasaidia kukabiliana na uzururaji na uzembe unaofanywa na baadhi ya vijana nyakati ambazo wanatakiwa kuwa shambani kulima mazao mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yao.

Mwanri alitoa kauli hiyo hivi karibuni Wilayani Kaliua wakati wa ziara yake ya kuhamasisha kilimo bora na ufanyaji wa kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alisema watu wanaoshinda wakicheza michezo mbalimbali wakati wenzao wako mashambani wakilima ndio wanakuwa wa kwanza kudai chakula cha msaada pindi wanapokabiliwa na njaa.

Mwanri aliwataka viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya hadi vitongoji kuhakikisha hakuna vijana ambao watakuwa mitaani wakicheza michezo mbalimbali wakati wanapaswa kuwa shambani.

Aliongeza kuwa  watu wa aina hiyo ndio wanasababisha ucheleweshaji wa maendeleo na wakati mwingine wanakuwa wa kwanza kuomba chakula cha msaada pindi wanapokuwa hawana chakula.

“Ni marufuku kucheza pool, karata na bao wakati huu…ni lazima watu wote wenye uwezo wa kufanyakazi wawe mashambani…michezo hiyo ianze nyakazi za jioni…tukiendekeza michezo hiyo nyakati za kilimo Tabora tutabaki watazamaji wa maendeleo wakati mingine inapiga hatua sisi tutabaki kulalamika kwa sababu ya kuendekeza michezo nyakati za kilimo” alisema.

Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa baadhi ya watu wa aina hiyo wakati mwingine ndio wanahisiwa kujihusisha na vitendo vya uharifu ikiwemo wizi na ukabaji kwa kuwa hawana shughuli ya kupatia kipato halali.

“Hivi kijana ambaye kila siku yuko kwenye bao, karata anapata wapi pesa za kujikimu yeye na familia yake ni lazima tujiulize…vijana ndio wazazi wa sasa wanajibika kubeba majukumu ikiwemo kufanyakazi kwa bidii kwa ajili ya ustawi wao na watoto wao”alisisitiza.

Alisema ni lazima kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi kuhakikisha kuwa anafanyakazi halali na kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha na kuwa na ziada itakayomsaidia katika shughuli za  maendeleo yake.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akionyesha mfano kwa vitendo kwa Wanakijiji wa Ibambo wilayani Kaliua juu ya palizi bora ya mimea wakati wa ziara yake ya siku nne ya kuhamasisha kilimo bora ikiwemo cha pamba hivi karibuni.


 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Dkt. John Pima akitoa ufafanuzi kabla ya ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ili atoea elimu kwa  Wanakijiji wa Ibambo wilayani Kaliua juu ya palizi bora ya mimea wakati wa ziara yake ya siku nne ya kuhamasisha kilimo bora ikiwemo cha pamba hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Pages