Baadhi ya wanahabari walio katika mradi wa mafunzo ya Nishati Jadidifu na wawezeshaji wakimuhoji wakala wa Kampuni ya Power Gen inayozalisha umeme wa jua, Malongo Maungo.
Kituo cha Kampuni ya Power Gen kinachozalisha umeme wa jua.
Na Happiness Mnale
NI miaka 24 sasa tangu wajumbe wa wanawake walipokwenda kudai usawa wa maendeleo Beijing.
Angalau sasa wanawake wengi wameweza kujikwamua kiuchumi na kuzalisha mali.
Katika
Kata ya Dongo, iliyoko Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, wanawake
wameweza kujikwamua kiuchumi baada ya umeme kufika katika kata hiyo.
Zena Mwambano, Mkazi wa kijiji cha Dongo, ni mama wa watoto wawili ambaye anafanya biashara ya vinywaji.
Anasema kwamba kupatikana umeme wa uhakika unaotumia nishati ya jua umemsaidia kuongeza thamani biashara yake.
“Awali
nilikuwa nafanya biashara hadi saa 12:00 jioni, lakini tangu kupatikana
kwa umeme ninafanya biashara hadi saa 5:00 usiku,” anasema.
Mwanamama huyo anasema anapata faida zaidi pindi anapopeleka vinywaji baridi kwenye minada inayofanyika kijijini Dongo.
Zena
anaeleza kwamba awali alipolazimika kufanya biashara hadi usiku
alitumia kibatari na wateja wake walikuwa hawapendi kutokana na moshi wa
mwanga huo.
Anakiri umeme huo kuwa na gharama kubwa hali iliyomlazimu kufunga mita kubwa.
“Awali
nilikuwa natumia mchana unit moja ya umeme kwa sh. tatu wakati wa
mchana na sh. sita kwa usiku,nikazungumza na wakala wa umeme akanishauri
nifunge mita kubwa,”
“Nilipofunga
mita kubwa gharama zikapungua mano mimi mchana nilikuwa natumia unit
tatu nikawa natumia unit moja na nusu,”anasema.
Amina Hassan mama wa miaka 57, naye najishughulisha na kuuza juice na barafu.
Kilio kikubwa cha Amina ni gharama za ununuzi wa umeme huo ambazo zinasababisha hapati faida kubwa.
“Kwasasa nimelazimika kufunga biashara ya kila siku bali nafanya siku ambazo kuna kuwa na wateja wengi,”
“Mfano
siku za mnada natengeneza juice na barafu ninauza, lakini sipati faida
kubwa kutokana na gharama za umeme kuwa juu,”anasema.
Lucy
Mwarabu anaendesha biashra ya kuchaji simu, anasema tayari pesa ya
kufunga umeme imesharudi na sasa anaendelea kupata faida.
“Fedha
nayopata kwa huduma ya kuchaji simu naitumia kununua daftari za watoto
na mahitaji mengine madogomadogo ya nyumbani kama kununua nyanya,
vitunguu,”
Kwa siku naingiza sh.800 hadi 1600, si haba si sawa na kukaa bure, naokota okota kidogo,”anasema.
Unapofika Kata ya Dongo utaona nyaya zilizosambazwa na nguzo kede zinazoshikilia nyaya hizo.
Kwa haraka unaweza ukadhani ni umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
La hasha, umeme uliosambazwa Kata ya Dongo na kutumiwa na vijiji viwili Dongo na Chang’ombe unatokana na nishati ya jua.
Umeme uo unasambazwa na Kampuni binafsi ya Power Gen, waliofunga mitambo yao katika kijiji cha Chang’ombe.
Tayari kaya 360 zimeunganishwa na umeme huo, usiokatika kabisa.
Isaac David, ni Ofisa Mtendaji Kata ya Dongo, anaeleza umeme huo ni rafiki licha ya kuwa na changamoto ya gharama kubwa.
Anasema kata hiyo haina umeme mwingine isipokuwa huo unaotokana na nishati jadidifu ya jua.
“Tulikuwa tunatumia mafuta na sola zile ndogo, lakini ulipokuja huu umeme tuliona mkombozi amefika,”anaeleza.
Anasema umeme huo pia umeunganishwa kwenye nyumba za ibada, shule, zahanati na kituo cha polisi katika kata hiyo.
Anasema
tangu umeme huo uunganishwe kijijini hapo wanawake wengi wamefaidika
kiuchumi kwa kuanzisha biashara ya mgahawa, vinywaji baridi, saloon za
kiume na za kike.
“Kwasasa
wanafanya biashara hadi usiku, wanawake wengi wa hapa kijijini
wameingia kwenye uzalishaji mali tangu umeme huu ulipofika,”
Anaeleza
kwamba Kata ya Dongo imekuwa na shughuli mbalimbali baada ya umeme
kuwepo ikiwemo biashara za mavazi ambazo zinafanyika hadi usiku, pia
kuangalia mechi za mipira kupitia rununga.
David anasema wanakabiliwa na changamoto ya umeme huo kuwa na gharama kubwa.
Anataja
changamoto kubwa ni kipato cha wakazi wa Dongo ambao wanategemea kilimo
na ufugaji kutoendana na gharama za kulipia umeme.
“Tunatamani umeme wa Tanesco ufike hapa kijijini ili gharama ziwe nafuu na kila mmoja autumie,”
“Lakini
pia hatuhitaji huu uondolewe maana wa Tanesco huwa unakatika katika
huko maeneo ambako upo, huu wa nishati ya jua haukatiki kabisa,”anasema.
Daudi Lonjole, anasema, anatamani kupata umeme huo lakini hana fedha za kuufunga nyumbani kwake.
“Wanaunganisha kwa sh. 30,000 nami sina uwezo lakini natamani kuwa nao niutumie kwa kupata mwanga na kupata habari,”anasema.
Wakala
wa umeme wa Power Gen, Malogo Maungo, anaeleza kwamba mitambo
iliyofungwa kijiji cha Chang’ombe, Wilaya ya Kiteto inauwezo wa
kuzalisha KW 16 lakini zinazotumika ni nusu.
Malogo anasema wana umeme mwingi lakini wateja ni wachache.
Kuhusu gharama kuwa juu anasema yeye hutumia sh. 35,000 kwa mwezi kwa kuwasha taa mbili na kuchaji simu akiwa nyumbani kwake.
Mhandisi
Victor Labaa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(Ewura) anasema umeme wazalishaji wadogo wa umeme ni kampuni binafsi
wenye uwezo wa kuzalisha KW 10 hadi KW ambao 100 wana ambao
wanaunganisha nyumba 30.
Meneja
Mradi na biashara wa kampuni ya Ensol, Prosper Magali anasema kampuni
yao imewekeza euro 400,000 (sawa n ash. Bilioni 102) katika uzalishaji
wa umeme wa jua wa KW 48 huko Mpale, Wilaya ya Korogwe mkoa wa Tanga.
Anasema wamesambaza umeme kwenye nyumba 200 lakini wanapata sh. milioni mbili pekee kila mwezi.
No comments:
Post a Comment