HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 22, 2019

WAKULIMA WA NYANYA KUPATA SOKO LA UHAKIKA-KAGERA

 Mfanyakazi wa Kiwanda cha kusindika nyanya cha  Victoria Edibles akiwa kazini.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Marco Elisha Gaguti, akizungumza na watendaji wa Kiwanda cha kusindika nyanya cha Victoria Edibles.



 Na Lydia Lugakila, Kagera

 Wananchi wa Kata ya Nyakibimbili Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wanatarajia kuondokana na changamoto ya zao la Nyanya kuozea sokoni na kushuka bei kila wakati baada ya Kiwanda cha kusindika zao hilo cha Victoria Edibles kilichogharimu bilioni 1.5 kukamilika kwa asilimia 100 tayari kwa kuanza uzalishaji.

Akikagua kiwanda hicho Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, amepongeza juhudi za mwekezaji wa kiwanda hicho cha kusindika nyanya  ambaye ni mbunge wa jimbo la Bukoba mkoani Kagera Mhe, Jason Samsoni Rweikiza, kwa namna alivyotatua changamoto ya wananchi mkoani humo walioteseka kwa muda mrefu kukosa soko la uhakika baada ya bidhaa hiyo yenye upatikanaji mkubwa mkoani humo kuwa nyingi sokoni hadi kuoza na kushuka bei jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wakulima wa nyanya mkoani Kagera.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa kiwanda hicho kimekuja kwa muda wa muafaka wakati ambao Rais Dkt. John Pombe Magufuli anahimiza Tanzania ya Viwanda.

Mkuu huyo amewataka wananchi kutumia vizuri uwepo wa fulsa hiyo na kuahidi ushirikiano mkubwa katika kiwanda hicho huku akimuhimiza mwekezaji na watendaji wa kiwanda hicho kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora, kuwa wabunifu ili kupata matokeo chanya.

"Bidhaa nyingi zipo sokoni lakini hazina viwango vinavyohitajika simamieni uzalishaji ili kupata matokeo ambayo yataleta tija kwa watumiaji" alisema Mkuu wa mkoa.

Ameongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utasaidia nchi mbalimbali kutumia bidhaa hiyo inayozalishwa mkoani humo.

Akielezea uwepo wa kiwanda hicho Mwekezaji Mbunge wa jimbo la Bukoba Mhe, Samson Rweikiza amesema kiwanda hicho kimeanzishwa mwaka 2016 kikiwa na malengo kuinua uchumi wa mkulima  mkoani Kagera na Tanzania kwa ujumla hasa baada ya kugundua wananchi wake wanalima nyanya lakini inaozea sokoni.

Mhe, Rweikiza amesema kiwanda hicho kimekamilika kwa 100% ambapo tayari maombi yashapelekwa TBS kwa ajili ya kupata alama na vibali na kuwa taratibu zote zimefanyika ambapo Chill sauce imepita kwa 100% bila vikwazo huku tomato sauce ikiwadaiwa vipengele kadhaa ambapo kimoja wapo ni punje za nyanya kuwa kubwa jambo ambalo linafanyiwa uboreshaji wa haraka.

"Wananchi limeni nyanya kwa wingi tayari kiwanda kipo biashara inaanza mara moja magari yapo ya kusomba na kusambaza bidhaa hadi mikoa mingine" alisema Rweikiza.

Kwa upande wake Afisa Masoko na Mauzo, Jafeti Kubebeka, amesema idara hiyo imejiandaa vyema kinachohitajika ni juhudi na kuhakikisha kwamba wanamudu ushindani unaokubalika sokoni na kuwaomba wananchi kuchamgamkia fulsa hiyo huku pongezi akizielekeza kwa Mwekezaji huyo kwa kufungua fulsa kubwa mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment

Pages