HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 05, 2019

WALIMU ARUSHA WAKUMBUKWA

Na Grace Macha, Arusha

WANANCHI wametakiwa kujenga tabia ya kuwakumbuka na kuwajali walimu waliofundisha kwani wana mchango mkubwa katika mafanikio waliyofikia.

Aidha, wametakiwa kujijengea utaratibu wa kuzitembelea shule walizowahi kupatiwa elimu na kuongea na waalimu na wanafunzi jambo linaloweza kuongeza hamasa kwa wanafunzi waliopo kuongeza juhudi kwenye masomo yao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na wanafunzi waliosoma shule ya sekondari ya kutwa ya Arusha kuanzia mwaka 1962 mpaka mwaka 1978 wakati walipofanya hafla fupi shuleni hapo ya kuwashukuru walimu wao, Materu na Redding.

Walimu hao, Mama Materu alikuwa mwalimu mkuu wa kwanza wa shule hiyo kuanzia mwaka 1963 mpaka 1982 walikula pamoja na wanafunzi wao ambao walipatiwa zawadi kama shukrani yakuwalea walipokuwa wadogo.

Mwenyekiti wa wafanyabiasha Arusha (TCCIA), Walter  Maeda alisema kuwa kuwatembelea na kuongea na wanafunzi shuleni hapo itawapa motisha wanafunzi wanaosoma kwa sasa kuona inawezekana kufanikiwa kupitia elimu hivyo waongeze bidii.

"Hii inawafanya wanafunzi waongeze bidii ili waje wawe kama Lowassa au OleNjolay au Maeda na wengine wengi hapa unaowaona hapa," alisema Balozi, Daniel Ole Njolay.

Alisema walipofika na kuona hali ya shule hiyo wameona hali halisi ya majengo na samani hivyo baada ya kuongea na waalimu wameona mahitaji yao hivyo wataenda kujipanga ili kuona namna ya kuisaidia shule hiyo.

Mwenyekiti wa wahitimu hao, Sambai Nailejileji, (70) alisema kuwa wamekutakana ili kuwapongeza waalimu hao ambao waliwafundisha miaka 50 iliyopita.

Mhitimu mwingine, Mathias Ole Kisambo,  kuwa ni vema wahitimu wengine wakarejea kwenye shule walizotoka na kushirikiama na jamii zilizopo huko katika kuboresha miundombinu na kuhamasizha vijana kujifunza zaidi.

"Tunaona sasa hivi walime wetu wana staafu wakifika miaka 70 au 80 hali yao inakuwa mbaya hivyo sisi wanafunzi ambao tunakuwa na uwezo kiasi ni vema tukawakumbuka kama tunavyowahudumia wazazi wetu kwani nao walitulea tukiwa shule," alisema OleKisambo.

"Hata kuona wanafunzi wangu wamefanikiwa kiasi hicho najivunia sana," alisema mwalimu Redding ambaye kwa sasa ni mkulima ambaye amejikita kwenye masuala yanayohusu baiolojia somo alilokuwa akifundisha.

Kwa upande wake mwalimu Materu ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1962 mpaka mwaka 1972 aliwashukuru wanafunzi wake kwa kumkumbuka na kuwaombea kwa Mungu azidi kuwabariki.

Wahitumu wengine walioshiriki hafla hiyo hi mwenyekiti wa TCCIA, Arusha, Walter Maeda, aliyewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa TANAPA, Lota Melamari, Mkurugenzi Mkuu hospitali ya AICC, Profesa, Sendui Ole Nguyaine na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

WALIMU WASHUKURU

Awali mwalimu mkuu wa shule hiyo, Christofa Malamsha aliwaeleza wanafunzi hao wa zamani kuwa shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa jengo la utawala.

Hivyo aliwaomba wanafunzi hao wa zamani kuwaongezea nguvu kwani kwa sasa wana kiasi cha shilingi milioni 50 walizozitenga kwa ajili ya kuanza ujenzi huo unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 250.

Mwalimu Malamsha alisema kuwa shule hiyo imezalisha watu mashuhuri na viongozi wakubwa hivyo anaamini wakiamua kusaidia ujenzi huo utakamilika ndani ya muda mfupi.

Aliwataka baadhi ya viongozi hao kuwa no Katibu mkuu mstaafu  wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Abdulrhman Kinana, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Mabalozi, OleNjolay na Dk Agustine Mahiga na wengine ambao ni wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi ambao hakuweza kutaja majina yao.

Kwa sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,600 kuanzia kidato cha kwanza ikiwa na idadi sawa ya wasichana na wavulana, waalimu 80 na wafanyakazi 10 wasio waalimu.

No comments:

Post a Comment

Pages