HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 22, 2020

Benki ya UBA yawapa shule wajasiriamali

Kutoka kushoto ni Allen Kimambo, Joseph Kusaga na Usman Isiaka, wakiwa katika semina ya kuelimisha wajasiriamali ili waweze kupeleka maombi ya ruzuku yenye tija kwenye Mfuko wa Tony Elumelu.


NA MWANDISHI WETU

BENKI ya UBA Tanzania imewanoa wajasiriamali watanzania ili waweze kuomba ruzuku ya mtaji wa biashara kutoka kwenye Mfuko wa Tony Elumelu (The Tony Elumelu Foundation (TEF).

Wajasiriamali hao walinolewa kwenye semina iliyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya uwezeshaji wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga na mnufaika wa TEF wa mwaka 2017 Allen Kimambo.

TEF ni mfuko wa hisani wenye lengo la kuwawezesha kiuchumi wajasiriamali wa Afrika.

Mfuko huo ulianzishwa na Tony Elumelu ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya UBA inafanya biashara katika nchi 20 barani Afrika na miji mitatu ya kibiashara ambayo ni London, New York na Paris.

Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa UBA Tanzania, Usman Isiaka, alisema TEF ni Taasisi ya hisani  barani Afrika katika masuala ya kuendeleza ujasiriamali kwa vijana.

Alisema kwa miaka 10 TEF imelenga kuwafikia vijana 10,000 wa Afrika ambao watatambulika, watafundishwa na kupewa mbinu za kufanya biashara ikiwemo kuwawezesha.

Isiaka alisema TEF itatumia Dola milioni 100 za Marekani ndani ya miaka 10 katika kuwezeshwa biashara za vijana wajasiriamali wa Afrika.

Kwa la TEF ni kutengeza mamilioni ya ajira barani Afrika kwa kuwawezesha vijana kupata mapato yanayohitajika ili kuwepo na maendeleo endelevu.

Falsafa ya TEF ni 'Ubepari Wakiafrika' inalenga kuinua mchango wa sekta binafsi katika ukuzaji uchumi wa Bara la Afrika huku ikisisitiza umuhimu wa kujenga utajiri katika jamii.

"Mpango wa kuendeleza ujasiriamali wa TEF uko wazi kwa wajasiramali wote wa Afrika wakiwemo wenye mawazo na biashara zinazochipukia au wenye mawazo ya biashara ambazo hazijafikisha miaka mitatu.

"...Watakaochaguliwa kutoka katika mchakato unaoendelea watajiunga na wenzao 9,000 kutoka nchi 54 za Afrika ambao wameshanufaika na mpango huu mpaka sasa.

"Washindi pia watapatiwa elimu ya jinsi ya kuendesha biashara zao, ushauri wakitaalam pamoja na ruzuku ya mtaji wa Dola 5,000 za Marekani kila mmoja," alisema Isiaka.

Alisema washindi pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wenzao duniani kote kwa kupitia mtandao wa TEF-Connect.

Alisema mwaka 2019 TEF ilipokea maombi 216,000 ambapo asilimia 42 yalitoka kwa wajasiriamali wanawake.

Alisema tangu kuanza kwa mpango wa TEF wa kuendeleza ujasiriamali mwaka 2015, wajasiriamali watanzania 189 wamenufaika kwa kupata elimu ya jinsi ya kuendesha biashara zao, ushauri wakitaalam na ruzuku ya mtaji vyote vikiwa na thamani ya Sh. Bilioni 4.3.

Akizungumza katika semina hiyo, Kusaga aliwataka wajasiriamali kuitumia vyema elimu hiyo ili kupeleka maombi yenye tija.

Mpaka hivi sasa TEF imewafundisha zaidi ya wajasiriamali 9,000 katika nchi 54 za Afrika. Wajasiriamali hawa wamepewa ruzuku za mitaji ya zaidi ya Dola milioni 45 za Marekani.

No comments:

Post a Comment

Pages