Mmoja wa wanaopatiwa matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu sugu akiwa anapatiwa huduma ya chakula hospitalini hapo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mawenzi ya Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jumanne Kiria.
Na Andrew Chale, Siha-Kilimanjaro
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni Nane (8) kwa ajili ya ujenzi wa Maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa ambukizi ikiwemo ya Kifua Kikuu katika Hospitali maalum ya Magonjwa ya kuambukiza Kibong'oto, mkoani hapa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dkt. Donatus Tsere wakati akizungumza waandishi wa habari pamoja na Maafisa Habari na Uhusiano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto walio kwenye ziara ya kuangazia mambo mbalimbali yaliyofanywa katika kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya awamu ya tano 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.
Dkt. Tsere alisema kuwa Serikali imetenga fedha hizo Bilioni 8 ambapo ujenzi wake tayari awamu ya kwanza umekamilika na hadi Januari 31 mwaka huu utakabidhiwa.
"Tunajenga Maabara kubwa ya kisasa itakayogharimu kiasi cha sh. Bilioni Nane ambapo ujenzi wake wa hatua ya kwanza umekwisha na wanakwenda hatua ya pili kukamilisha ujenzi huo na kuanza kutumika ifikapo 2021."
"Maabara hii itakuwa ni ya kisasa kwa Afrika Mashariki na itakuwa ikipima magonjwa yote ambukizi ambapo pia itakuwa na uwezo wa kuhifadhi data za sampuli zaidi ya miaka 20.
Lakini pia itakuwa ikitumika na kufanyia utafiti wa magonjwa hayo na hii itasaidia kupata wataalam wengi kuja kufanya utafiti hapa" alisema Dkt. Tsere.
Dkt.Tsere alibainisha kuwa, kutokana na Serikali kuwekeza katika Hospitali na Vituo vya Afya 145, Kibong'oto inapokea wagonjwa ambao wana kifua kikuu sugu ambao wanapatiwa matibabu hapo kwa muda maalum.
"Kwa sasa idadi imepungua kutokana na vituo hivyo. Hadi leo tunawagonjwa wanaofikia 70 ambao wanakifua kikuu sugu. Awali tulikuwa tunawagonjwa kati ya 70 hadi 120.
Aidha, Dkt. Tsere alisema Serikali inakuja na mpango wa kuibadilisha Hospitali hiyo kuwa Taasisi kubwa itakayoweza pia kutoa tiba na kufanya tiba na tafiti.
"Hospitali ya Kibong'oto itakuwa Taasisi kubwa ya Magonjwa ambukizi na afya ya jamii ambapo itakua kitovu cha utafiti,tiba na mafunzo ya magonjwa hayo ya kuambukiza na magonjwa ya jamii.
Hivyo pamoja na ujenzi huo wa maabara ya kisasa tunamshukuru sana Rais kwa kuweza kuongeza uboreshaji sekta ya Afya kwa vitendo" alisema Tsere.
Pia alibainisha kwamba, katika utoaji wa majibu yanayotolewa katika Hospitali hiyo yamepata Ithibati na Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Maabara yetu inawatalaam wabobezi na tunavifaa vya kisasa. Majibu yanayotoka hapo ni uhakika hata ikitokea mtu aende hospitali yeyote majibu hayo hayawezi kubadilika.
Uwekezaji wa vifaa vya maabara vya uchunguzi wa vimelea vya Kifua Kikuu Sugu kumefanya kutoa majibu ndani ya masaa mawili tofauti na awali majibu yalikuwa yanatoka kwa masaa 24 hali ambayo ilikuwa inafanya kukaa kwa sampuli kwa muda mrefu."
"Serikali imerahisisha utoaji wa huduma kwa kuleta vifaa vya kisasa huku maboresho mengine yakiendelea kufanyika ikiwa ni kuhakikisha jamii inapata huduma bora za afya na kuongeza watalaam wakiwemo Madaktari, Wauguzi na wataalam wa maabara.”alisema Tsere.
Ambapo alieleza kati ya wagonjwa 300 waliopima kifua kikuu Sugu (TB) asilimia 20 walipatikana kuwa Kifua Kikuu Sugu pamoja na virusi vya Ukimwi.
Hospitali Maalum ya magonjwa yakuambukiza Kibong’oto ilianzishwa mwaka 1925 na Dkt. Noman Davis (raia wa Uingereza) ikiwa ni kituo cha kutibu watu waliokuwa wanaugua ugonjwa wa Kifua Kikuu na mnamo mwaka 2006 Wizara ya Afya iliipa jukumu Hospitali hiyo kutibu ugonjwa sugu wa Kifua Kikuu hadi sasa hospitali hiyo inatoa huduma ya tiba na uchunguzi kwa wagonjwa wa nje na ndani wa Kifua Kikuu huku wastani wagonjwa 120 wa nje na 110 wa ndani hupatiwa huduma za matibabu kila siku.
No comments:
Post a Comment