HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 27, 2020

Floresta yagawa mbuzi, fedha kwa vikundi vya kilimo hai

 Mkurugenzi wa Shirika la Floresta Tanzania, Richard Mhina (katikati) akitaja majina ya vikundi vilivyoshinda na kupata zawadi kutoka Floresta. Kulia ni Dk. Mkindi na kushoto ni Mkurugenzi wa SAT, Janet.
Nembo ya ubora inayowekwa kwenye mazao yatokanayo na kilimo hai.
Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania, Dk. Jackline Mkindi akikabidhi zawadi ya cheti kwa mkulima mshindi wa utengenezaji wa mbolea bora ya mboji.
 
  
 Na Irene Mark

SHIRIKA la Floresta Tanzania limetoa zawadi za mbuzi wa maziwa zaidi ya 170; fedha taslim Sh. milioni 3.1; vitabu vya kilimo hai kwa shule za sekondari, msingi na vikundi vya kilimo hai na utunzaji wa mazingira.

Hafla ya utoaji wa zawadi hizo ilifanyika hivi karibuni kwenye viwanja vya Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ikishirikisha vikundi 365 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Kabla ya ugawaji wa zawadi hizo, wakulima na wafanyabiashara wa kilimo hai walipata fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao huku wakitoa elimu kwa maelfu ya wakazi wa mji huo na wageni kutoka ndani na nje ya nchi walihudhuria maonesho hayo ya kila mwaka.

Akikabidhi zawadi ya cheti, kombe, fulana, mbuzi wa nne na viti 50 vya plastiki, kwa mshindi wa jumla ambaye ni kikundi cha Kwasembala, Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania Dk. Jacline Mkindi, alisema mazao ya kilimo hai ni mlango wa kipato na afya njema kwa mkulima na mlaji pia.

Dk. Mkindi aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maonesho hayo alielez namna mazao ya kilimo hai yanavyohitajika sokoni kwa bei kubwa kwa kuwa dunia imegundua athari kubwa za kiafya zinazowapata wakulima na walaji wa mazao yanayotokana na mbolea zenye kemikali sumu za viwandani.

"Lengo kuu la Floresta ni kuhamasisha wakulima kuhifadhi mazingira, kuzalisha matunda, mboga na vyakula kwa njia asili bila kutumia mbolea zenye kemikali sumu zinazotengenezwa viwandani.

"...Lakini pia kuwaunganisha  wakulima Hawa na masomo ya mazao hai ili waboreshe vipato vyao na kuondoa umaskini wa kiuchumi kwenye familia zao na taifa," alisema Dk. Mkindi.

Alisema ulaji wa mazao ya kilimo hai licha ya kuongeza kipato unakupa uhakika wa afya kwa kuepuka maradhi ya saratani, figo na kisukari ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na ulaji wa kemikali za viwandani zinazotumika shambani.

"Takwimu zinaonesha sekta ya kilimo hasa matunda na mbogamboga inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa taifa.

"Uzalishaji wake umeongezeka kutoka tani 40,602 mwaka 2001/2002 hadi tani 92,250 mwaka 2007/2008 hivyo mauzo kwa fedha za kigeni kuongezeka kutoka Dola za Marekani 63,400 hadi 140,000 huku ikichangia ongezeko la ajira ya watu 12,000 waliokuwepo mwaka 2006 hadi wakulima 20,019 mwaka 2009," alisisitiza Dk. Mkindi.

Alitumia nafasi hiyo kuzishauri idara za Kilimo, Mazingira na Maji ngazi ya halmashauri kufanyakazi kwa karibu na mashitaka binafsi likiwemo Floresta ambalo kazi zake zinaonekana na kutoa kipaumbele kwa kutenga bajeti kuhamasisha kilimo hai cha mbogamboga na matunda.

Mkurugenzi wa Floresta Tanzania, Richard Mhina alisema shirika hilo ni mwanachama wa Shirika la Kuendeleza Kilimo hai Tanzania (TOAM), huku akibainisha kwamba ni azma ya Floresta kuongeza idadi ya vikundi vya kilimo hai mkoani humo.

"Leo tumetoa zawadi kwa mkulima mmoja mmoja waliofanya vizuri kwenye uoteshaji na utunzaji wa miti na utengenezaji wa mbolea ya mboji.

"Kwenye vikundi waliopata zawadi ni waliohitimu mafunzo ya utunzaji wa mazingira na kilimo hai na waliopo mafunzo lakini pia tunawapa hamasa ya kufanya vizuri zaidi," alisema Mhina.

Kwa mujibu wa Mhina, kila mwaka tunapanda miti milioni 1.5 na asilimia 70 inaota na inaendelea vizuri, lengo ni kuufanya Mkoa wa Kilimanjaro kuwa na mazingira bora na wakulima wake kufanya kilimo hai.

 

No comments:

Post a Comment

Pages