Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza wakati wa kufunga semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameviagiza
vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinawalinda wafanyabiashara wa
madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata sheria na kujiepuka kamata
kamata zisizo na tija.
“Katika
kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa
wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila
sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea
suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo
kufuata taratibu.”
Ametoa
agizo hilo leo (Jamapili, Januari 26, 2020) wakati akifunga semina ya
ushiriki wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika usimamizi na udhibiti wa
rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu amesema kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatakiwa vitumie
Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya
kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuviagiza vyombo vya Dola kusimamia na
kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha kuwa masoko yote ya
madini nchini yanalindwa.
“Nyote
mtakubaliana nami kwamba kila taasisi ina utaalamu na wataalamu wake.
Kwa hivyo, hatunabudi kufanya kazi kwa kuheshimu na kutambua utaalamu
ama taaluma za wengine tunaoshirikiana nao.”
“Sasa
ni vema tukaondoa tofauti zetu na kuwa kitu kimoja kwa lengo la
kuimarisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali madini. Aidha, tutambue
kuwa kuna nyakati hatuhitaji kutumia nguvu nyingi bali ushauri tuu ili
kutatua changamoto husika.”
Waziri
Mkuu ameelekeza kwamba kuanzia sasa wadau wote wanaopatikana na madini
wapewe utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza madini hayo badala ya
kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni.
Waziri
Mkuu amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa
yote ya Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema
walikosa msaada wa kitaalamu. “Ni wajibu wetu sote kama watumishi wa
umma kujenga mazingira rafiki ya kazi, kuaminiana na kufanya kazi kwa
ushirikiano.”
Wakati huo huo,Waziri Mkuu amesema kuazia sasa suala
la migodi kutegemea bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi lifikie ukomo
kwa kuhakikisha kuwa, kila huduma inayohitajika migodini, inapatikana
nchini.
Waziri
Mkuu amesema nchi inawajibu wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya
wadau wa madini kwa maana ya kutoa huduma kwa ubora stahiki na kwa
wakati muafaka.
Amesema
sekta ya madini inazalisha ajira ila kuna changamoto ya ubora wa ajira,
mishahara na stahiki katika kazi zinazofanana na suala la unyanyasaji
wa wafanyakazi.
Waziri
Mkuu amesema masuala mengi hapo yanaweza kuonekana haraka kwenye maeneo
yao ya kazi, hivyo ni vyema wakawa na taarifa hizo kwa wakati na
kuwasilisha kwa wahusika ili mambo yawekwe sawa na kuipeleka sekta
mbele.
Akizungumzia
kuhusu suala la unyanyasaji wa wafanyakazi wazalendo amesema si suala
la kufumbiwa macho kama ilivyo suala la usalama wa watenda kazi katika
migodi.
Kadhalika,
suala la udhibiti wa wageni kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na
Watanzania wenzetu pia ni jukumu letu na hivyo ni wajibu wetu kusimamia
mikataba tuliyoingia na wawekezaji hususani eneo la urithishaji wa
madaraka na ujuzi kwa wazawa.
Kwa
upande wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Waziri Mkuu amewaagiza
watafute suluhu ya changamoto ya usalama wa wafanyakazi kipindi wakiwa
kazini na baada ya kumaliza muda wa kazi kwa hiari au kwa kustaafu au
kumaliza mkataba. “Tumepokea malalamiko mengi sana katika eneo hilo.”
“Hivyo,
ni wajibu wetu kushirikisha wadau wote wanaohusika na masuala ya ajira,
bima za wafanyakazi, afya za wafanyakazi na usimamizi wa stahiki za
wafanyakazi kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto hii ili isiendelee
kukomaa.”
Vilevile,
Waziri Mkuu ameagiza suala la utunzaji wa mazingira liwekewe mkazo wa
kipekee maana nje ya mazuri yote yaletwayo na Sekta ya Madini, uharibifu
wa mazingira unaweza kugharimu maisha ya binadamu, wanyama na mimea.
Waziri
Mkuu amesema “mazingira yetu ndio uhai wetu sisi na vizazi vijavyo,
hivyo ni wajibu wetu kama Wizara kuhakikisha wawekezaji wetu ni watu
wema kwa mazingira yetu.”
Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza
na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu mkubwa
alioufanya ambao umeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya madini.
“Hili
linadhihirishwa na kitendo cha utiaji saini makubaliano ya uanzishwaji
wa Kampuni ya Twiga Minerals uliofanywa juzi Jijini Dar es Salaam tarehe
24 Januari 2020 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini
ya mwaka 2017.”
Awali,
Waziri wa Madini Doto Biteko alisema lengo la semina hiyo ni kujenga
uelewa wa pamoja kwenye masuala ya usimamizi wa sekta ya madini nchini.
Alisema
suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini linafanyika kwa kushirikiana
kati Wizara ya Madini na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwamba
wanaendelea kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza.
Waziri
Biteko ametumia fursa hiyo kutuma salamu kwa wafanyabiashara
wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa madini bandia pamoja na
wanaotaka kuuza madini nje ya mfumo kuwa zama zao zimekwisha.
No comments:
Post a Comment