Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akichomoa moja ya Majalada ya Ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Mpanda
jana akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika
mkoa wa Katavi. (Picha na Wizara ya ya Ardhi) .
Na Munir Shemweta, WANMM UVINZA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameijia juu halmashauri ya
wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma kwa kushindwa kuihudumia idara ya ardhi na kusababisha
watumishi wa idara hiyo kugharamia baadhi ya vifaa ili kutekeleza majukumu yao.
Hali hiyo ilibainika jana
katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi
katika mkoa wa kigoma.
Akiwa katika Masijala ya
Ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Uvinza, Dkt Mabula alibaini utunzaji majalada
ya ardhi usiofuata taratibu huku baadhi ya hati zikiwa hazijakamilishwa kwa
ajili ya kuwapatia wamiliki wa ardhi katika halmashauri hiyo tangu mwaka 2018.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika
halmashauri hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo jambo alilolieleza
kuwa linachangia uwepo migogoro ya ardhi sambamba na kuwanyima wananchi fursa
ya kupata hati.
Dkt Mabula aliagiza hati
zote ambazo taratibu zake zishakamilishwa ikiwemo wamiliki wake kusaini hati
hizo kupelekwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi ndani ya
wiki moja kwa ajili ya kukamilishwa na
kupatiwa waombaji.
Hata hivyo, baada ya
kuwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Uvinza ndipo
Afisa Ardhi wa halmashauri hiyo Manyama Makongo alipomueleza kuwa idara hiyo
inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosa vifaa jambo lililosababisha
kuamua kuchukua ‘Printer’ yake binafsi na
kuipeleka kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kusaidia kazi za idara.
Hali hiyo siyo tu ilimshutua
na kumshangaza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi bali
ilimsononesha kwa kuona watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo
wanatumia fedha zao za mifukoni kuendesha ofisi jambo alilolieleza kuwa
halikubaliki.
‘’Hapa jitihada za ziada
zinahitajika, halmashauri ipo inashindwa kuihudumia idara ya ardhi, halafu
watumishi wanatumia fedha zao za mfukoni hili halikubaliki lazima niwasiliane
na Waziri Jafo kuhusiana na suala hili’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri Mabula, idara za ardhi katika halmashauri nyingi nchini zimekuwa kama
watoto wa kambo kutokana na wakurugenzi wa halmashauri kutozitengea bajeti ya
kutosha jambo linalofanya idara kufanya kazi katika mazingira magumu.
Katika
hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi
Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Enelia
Lutungulu wamewaokoa Maafisa Ardhi wa halmashauri hiyo wasitumbuliwe kutokana
na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutokamilisha utoaji wa hati
za ardhi kwa muda mrefu.
Walionusurika ni Afisa Ardhi
Mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Spear Mwalukasa ambaye ilielezwa
yuko katika mafunzo na Afisa Ardhi Ezekiel Bichuro. Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema kutokana na
Maafisa hao kuzembea kukamilisha hati kwa muda mrefu basi hawafai kuendelea na
nafasi zao kwa kuwa wanakwamisha utoaji hati ambao sasa unaweza kufanyika ndani
ya mwezi mmoja pale taratibu zote zinapokuwa zimekamilika.
Hata hivyo, Mkuu wa
wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi Enelia Lutungulu waliwatetea
kwa kueleza kuwa maafisa hao hawana muda mrefu katika idara hiyo na makosa yanaweza
kuwa yalifanywa maafisa waliopita.
Naibu Waziri Mabula
alielekeza maafisa hao kupewa barua za onyo kwa kuwa muda wa miezi mitatu waliopo
katika idara hiyo wangeweza kuonesha jitihada za kukamilisha hati na kuagiza hati
zilizopo zikamilishwe katika kipindi cha mwezi mmoja.
‘’Ikifika tarehe 30
Januari 2020 hati ziwe zimeenda kwa wenyewe, haiwezekani mtu amesaini tangu
2015 halafu mpaka sasa hajapatiwa hati yake, wapo wazembe wachache wanaochafua Wizara lazima wapewe warning.
Alisema Naibu Waziri Mabula.
Naibu Waziri Mabula pia
alitembelea wilaya ya Tanganyika ambapo alionesha kutoridhika na kasi ya
ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi na kuagiza halmashauri
ya wilaya ya Tanganyika kuongeza kasi katika makusanyo sambamba na kupanga,
kupima na kumilikisha viwanja kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Afisa Ardhi
wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Penina Simon kiasi cha shilingi milioni
18,069,179.40 kilikusanywa hadi kufikia nusu ya mwaka wa fedha 2019/2020.
No comments:
Post a Comment