HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2020

IGUNGA YAKISIA KUKUSANYA BILIONI 45.9 MWAKA UJAO WA FEDHA

NA TIGANYA VINCENT

HALMASHAURI ya Wilaya ya Igunga imependekeza ya makisio ya mapato na matumizi ya zaidi shilingi bilioni 45.9  kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/21.

Fedha hizo zinatarajia kutokana na makusanyo ya vyanzo mbalimbali ikiwemo ruzuku toka Serikali kuu na makusanyo yanayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilya ya Igunga Joel Nkesela wakati wa kikao na Sekretaieti ya Mkoa wa Tabora cha kuchambua na kujadili mapendekezo ya makisio ya mipango na bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa mwaka ujao wa fedha wa 2020/21.

Alisema kati ya fedha hizo bilioni 42.7 ni ruzuku kutoka Serikali kuu  na bilioni 3.1  zitatokana na makusanyo yanayotokana na mapato ya ndani.

Nkesela  alisema mapendekezo ya bejeti ijayo yamezingatia uimarishaji wa makusanyo ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kuongeza vyanzo vya mapato vipya ili kuongeza mapato.

Aliongeza kuwa vipaumbe vingine ni pamoja kuboresha huduma za afya na elimu ya awali hadi kidato cha nne na kuimarisha miundombinu ya utoaji elimu na lishe kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Nkesela alisema pia wanakusudia kuendeleza kilimo cha mpunga kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Hamis Mkunga aliwataka viongozi wa Halmashauri hiyo kujitahidi kubuni na kuimarisha vyanzo vipya wa mapato ili wawe na  uwezo wa kujitegemea ifikapo mwaka 2025 kama Serikali ilivyoagiza.

Alisema sanjari na hilo ni vema wakaanza kutenga fedha katika bajeti yao kwa ajili ya  ununuzi  ardhi ambayo wataipima kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali ambao utawasaidia kwenye uongezaji wa mapato kwa Halmashauri na pia kutoa ajira kwa wananchi. 

Mkunga alisema miaka imebaki michache kufika 2025 ni vema wakaongeza kazi katika mipango yao ya kuwa na vyanzo vya mapato vingi ambao vitawasaidia kupata fedha za uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi.

Kwa upande wa Katibu Tawala Msaidizi  Mkoa wa Tabora Rukia Manduta alizitaka Halmashauri zote ikiwemo Igunga ambazo haziwalisha andiko la miradi ya Kimkakati kuandika haraka ili waweze kuomba fedha ambazo zitawasaidia katika utekelezaji wa mradi waliopanga kwa ajili ya kujiongezea mapato yao ya ndani pindi utakapokuwa umekamilika.

No comments:

Post a Comment

Pages