HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 25, 2020

KAMPENI YA CHOO BORA YAPIGA HODI MKOANI KAGERA

Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Desdery Karugaba.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Bablus Mashauri, akizungumza na wadau katika kikao cha lishe.
 
 
Na Lydia Lugakila, Bukoba

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Bablus Mashauri, amemuagiza Afisa Afya Mazingira wilayani humo, Clara Macha, kuhakikisha anafanya jitihada za haraka kunusuru kaya ambazo hazina vyoo bora.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Bablus Mashauri katika kikao cha lishe kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani humo.

Akitaja kusikitishwa na hali ya kutokuwa na vyoo bora katika baadhi ya kaya zilizopo halmashauri ya wilaya hiyo mkurugenzi huyo amesema kwa malengo ya kitaifa ya kaya zenye vyoo bora ni 75% ambavyo wilaya hiyo imefikia 34% tu hivyo kumuagiza afisa afya mazingira wilayani kusimamia haraka  maelekezo ya serikali ya ujenzi wa vyoo
Bora kwa kila kaya.

Alipohojiwa Afisa Afya, Clara Macha juu ya hali hiyo amesema hii ni kutokana na uwezo mdogo wa wananchi jambo ambalo kaimu mkurugenzi huyo hakutaka kulisikia.
"Unasema uwezo mdogo ndio unaowafanya wananchi kutokuwa na vyoo bora sitaki kusikia suala hilo uwezo wao umeupimaje? Mwananchi awe na nyumba nzuri alafu choo ni ya mabanzi inaonesha uchafu kweli Nani akubali hali hiyo? alihoji kaimu mkurugenzi huyo".

Mashauri amemuagiza afisa afya mazingira huyo kujipanga kikamilifu kwa kushirikiana na idara ya mahakama kuchukua walau kijiji kimoja katika Kaya ambazo hazina vyoo bora kwenye sheria li iwe mfano kwa wengine kwani kiafya suala hilo lina miongozo.

Amesema choo bora haina gharama na wala suala hilo halina cha uwezo mdogo kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu.

Kaimu mkurugenzi huyo amemtaka Bi Clara kutumia sheria ili kuwakumbusha wananchi kuwa na vyoo bora.

Amesema awali Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenarali Marco Elisha Gaguti alifanya uhamasishaji wa kutosha kwa kuambatana na wasanii mbalimbali wa Tanzania akiwemo Mrisho Mpoto ambapo mkuu huyo wa mkoa alitoa miezi mitatu ambayo tayari imepita na vyoo bado na hadithi.

 Amesema Mkoa wa Kagera una heshima zake hivyo hakubali kuona unaangushwa na mambo madogo kama hayo na kutaka ifanyike kampeini ya haraka ili kunusuru kaya hizo zilizopo hatarini.

Ameeleza kuwa upande wa afya sheria inaruhusu wataalamu kushtaki moja kwa moja mahakamani kwa wale wasiotii maelekezo ya serikali katika masuala ya afya.

Naye Afisa Afya Mazingira, Clara Macha, amemhakikishia kaimu mkurugenzi huyo kuwa, kupitia wahudumu ambao ni  watendaji wa kata na vijiji pamoja maafisa afya katika kata hawakwami katika uhamasishaji.

Hata hivyo Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Desdery Karugaba, amesema wilaya hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika masuala mbali mbali ya lishe kwa makundi mbali mbali na kufanikiwa ikiwemo kupangilia bajeti na kufanikiwa huku akieleza kuwa kati ya uhamasishaji ambao umekuwa ukifanyika ni pamoja na kaya zote kuwa na vifaa vya kunawia mikono  na kaya zote kuwa na vyoo bora huku Halmashauri hiyo ikiendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe kadri ya mkataba wa utendaji kazi wa shughuli hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages