HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 12, 2020

Kubenea amvaa Mkurugenzi sakata la Umeya wa Jiji Dar

Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, kuhusu sakata la kumng’oa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita. (Na Mpiga Picha Wetu).
 

Na Irene Mark

MBUNGE wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema), amesema Ofisi za Meya wa Jiji la Dar es Salaam, hazitakalika wala kufanyika shughuli zozote za utendaji endapo Mkurugenzi wa Jiji Sipora Liana, hatomtambua Issaya Mwita kuwa Meya halali wa Jiji hilo.

Pamoja na kauli hiyo aliwataka wote wanaotamani kumuondoa Mwita waanze upya mchakato wa kutengeneza mashitaka dhidi ya Meya huyo ama wamuombe Rais John Magufuli aivunje Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na si vinginevyo.

"Kama yote hayo yatashindikana basi watambue kuwa jiji halitatawalika bila Meya Mwita. Hatutakubali hata ngumi tutapigana," alisisitiza Kubenea.

Akiwa na nyaraka mbalimbali alizozitumia kufanya rejea kwa  waandishi wa habari aliozungumza nao leo Januari 12,2020 ofisini kwake Kinondoni, Kubenea alimtupia lawama Liana kwa madai ya kutojua mipaka ya utendaji wake na kughushi.

Alisema mkurugenzi huyo aliandika kwenye orodha ya mahudhurio jina la diwani ambaye hakuwepo kabisa Dar es Salaam ili kufanya udanganyifu wa kuongeza idadi ya wajumbe watakaokidhi akidi ya wapigakura wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliopanga kumng'oa Meya wa Jiji.

"Mkurugenzi alikuwa sehemu ya vurugu kwenye kikao kile ambacho kwangu sio halali, baraza la madiwani wa Jiji wenye uwezo wa kuamua kuhusu Meya lina wajumbe 26 na ili jambo liamuliwe na likubalike kisheria lazima itimie theluthi mbili ya wajumbe wote.

"...Theluthi mbili ya 26 ni 17 na siku ya kikao tulikuwa wajumbe kwa maana ya madiwani 18 kati yao wawili ambao ni mimi na Boniface Jacob Meya wa Ubungo tumetoka Chadema tuliikataa hoja yao wakabaki 16 ambao ni CCM, kwa idadi yao kisheria hawatoshi kuamua lolote juu ya kumuondoa Meya wa jiji," alisema Kubenea ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha kwenye Baraza la Madiwani wa Jiji.

Mbunge huyo aliendelea kumtupia lawama mjumbe mwenzie wa baraza hilo, Abdallah Chaurembo kuwa ndiye kinara wa fujo aliyeandika mashitaka ya kutokuwa na imani dhidi ya Meya Mwita na kupeleka kwa mkurugenzi Liana.

"Chaurembo hana 'moral authority' ya kuzungumzia utendaji wa Meya ninamjua vilivyo na uwezo wa kunigusa hana, mimi sio wale niguse ninuke... mimi niguse tunuke," alisema Kubenea ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.

Aliyataja baadhi ya mashtaka ya Chaurembo dhidi ya Meya kuwa ni matumizi mabaya ya gari la ofisi, kushindwa kufanya matumizi ya fedha za hisa za Uda ambazo ni zaidi ya Sh. Bilioni tano, kuwaingiza mameya wa manispaa zote za Dar es Salaam kwenye Kamati ya Fedha ya Jiji na kushindwa kuzuia vurugu zinazotokea kwenye mikutano.

Majibu ya Mkurugenzi


Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Kubenea, Mkurugenzi wa Jiji, alimtaka  mbunge huyo wa upinzani kumpeleka kwenye Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iwapo anaamini  alicheza mchezo mchafu kwenye sakata la kumuondoa Mwita.

"Asilalamike tu achukue hatua aende TAKUKURU kunishtaki kama nimeghushi jina la diwani na kuhusu kutokubaliana na uamuzi wa kuondolewa madarakani Kwa Meya Jacob, namshauri akate rufaa kwa Waziri wa Tamisemi," alisema Liana.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Meya Mwita alipewa barua na Mkurugenzi wa Jiji ikimtaka  kukabidhi ofisi ndani ya siku 14 baada ya kung'olewa madarakani.

No comments:

Post a Comment

Pages