HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 30, 2020

Maalim Seif aanza mbio urais Zanzibar

Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, akionesha fomu ya kugombea nafasi ya uwenyekiti wa Taifa wa chama hicho baada ya kukabidhiwa na Kaimu Katibu Mkuu,  Doroth Semu, katika Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Vuga, Zanzibar. (Picha na Talib Ussi).
 


Na Talib Ussi, Zanzibar

MSHAURI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amechukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho utakaofanyika Machi mwaka huu.
Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi na baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), alichukua fomu hiyo jana katika ofisi za chama hicho Mtaa wa Vuga  mjini Unguja.

Hatua ya Maalim Seif kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti ndani ya chama hicho imeelezwa kuwa ni hatua moja kuelekea kugombea urais wa Zanzibar mwaka huu.

Kama hilo litafanyika, itakuwa ni mara ya sita kwa Maalim Seif kugombea urais wa Zanzibar ingawa mara zote alikuwa akigombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF) ambacho alikihama mwaka jana baada ya kukumbwa na mgogoro wa muda mrefu uliokigawa pande mbili, Maalim Seif kama Katibu mkuu na Profesa Ibrahim Lipumba akiwa mwenyekiti wa chama hicho.

Akitoa sababu za kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo nyeti ndani ya chama alisema ni baada wapenzi na wanachama kumwomba kufanya hivyo.

“Nimeona kama sikugombea nafasi hii wafuasi na wanachama ambao walisema nilipo wapo sitawatendea haki na hawatanielewa  na nitakuwa nimewavunja moyo,” alisema Maalim Seif.

Aidha, aliitaja sababu ya pili  kuwa anataka apate nafasi  ya kutoa mchango wake wa kuleta maendeleo katika chama hicho kwa kushirikiana na wenzake.

“Uzoefu ninao, uwezo pia na wanachama wananipenda kwa nini nisiombe nafsi ya kuongoza chama chetu?” alieleza Maalim seif.

Alieleza kuwa kwa kushirikiana na viongozi pamoja na wanachama wataweza kuleta maendeleo makubwa pamoja na kujenga  maelewano baina ya wanachama, viongozi na hatimaye kupata uongozi wa kuwajibika kwa kushirikiana.
Aidha, alisema kuwa anategemea chama chao kitaweza kuchukua halmashauri na majiji mengi katika pande zote za muungano.

“Kwa kushirikiana na wenzangu tutajenga chama ambacho kitakuwa na wanachama wengi ndani ya Tanzania na kuchukua masikio  ya watu ndani na nje ya nchi, nataka ifikapo mwaka 2025 chama kiwe kinaongoza halmashauri za wilaya na miji mingi na kuwa sehemu ya uongozi wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hiyo ndiyo ACT – Wazalendo ninayotaka kuijenga kwa kushirikiana na wenzangu pindi wakinipa ridhaa ya kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema.
Kuhusu kugombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif aliwaeleza waandishi wa habari kwamba muda ukifika ataeleza lakini kwanza ameanza na nafasi hiyo.

“Muda ukifika chama chetu kitatangaza kama hivi uchaguzi wa ndani na muda ndio nitaeleza kama nina nia au la,” alisema bila kufafanua.

Uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali ACT-Wazalendo umeanza Januari 27 na unatarajiwa kukamilika  Februari 27 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages