HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2020

Mgalu: Mikoa mitano kupata gesi asili

 Naibu Waziri Subila Mgalu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa Serikali kwa kushirikiana na JICA kupeleka gesi kwenye mikoa mitano.
Mshauri wa Taasisi ya Nishati na Uchumi kutoka Japan, Kensuke Kenekinyo akielezea mpango huo uliofanyika kwa miaka mitatu.
 

Na Irene Mark

SERIKALI imekamilisha mpango wa awali wa kusambaza gesi asili kwenye mikoa mitano ili kuhakikisha Tanzania inatumia rasilimali hiyo kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema mpango huo ni matokeo ya utafiti wa miaka mitatu, uliofanywa na Serikali kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA).

Mgalu aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro huku akibainisha kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha mikoa yote Tanzania inapata nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali.

"Tanzania tumegundua gesi asili yenye ujazo wa futi trilioni 57 hii sasa tunaitengenezea mkakati wa matumizi yake, mpaka sasa gesi asili inazalisha megawati 800 za umeme kati ya megawati 1,601 za umeme zinazohitajika.

"...Gesi hii asili I natumika pia kwenye magari, tumeanza hapa Dar es Salaam ambapo magari takribani 200 yanatumia gesi na miundombinu ya kusambaza gesi inaendelea na ndio maana hasa ya utafiti huu.

"Gesi asili inatusaidia pia kutunza mazingira hasa kwenye kupikia ambapo mpaka sasa Shirika la Petroli (TPBC), limesambaza miundombinu ya gesi ya kupikia majumbani kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani," alisema Naibu Waziri Mgalu.

Kuhusu matumizi ya gesi viwandani Mgalu alisema viwanda zaidi ya 50 vimeunganishwa na gesi asili ili kusaidia uzalishaji wa mbolea.

"Huu ni mradi mkubwa tunategemea lifespan yake kuwa ya muda mrefu pia hadi mwaka 2046 tangu kuanza kwa mradi huu mwaka 2017.

Kamishna wa Maendeleo ya Petroli na Gesi, Adam Zuberi alisema Tanzania ipo kwenye wakati sahihi hivyo jitihada za makusudi zinafanyika kufikisha gesi asili kwenye mikoa yote Tanzania.

"Tupo on truck hii study inalenga kuhakikisha mikoa yote inapata gesi asili kwa njia sahihi... huu ni mwanzo tutafika mikoa yote nchi nzima," alisema Zuberi.

Mshauri wa Taasisi ya Nishati na Uchumi kutoka Japan, Kensuke Kanekinyo alisema awamu ya kwanza ya mradi huo imetumia Dola Milioni mbili za Marekani kwa miaka mitatu.

Alisema gharama za mradi wote ni Dola milioni 250 zitakazotumika kupeleka gesi mikoa yote.

No comments:

Post a Comment

Pages