Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa Khalfan Haule (kulia) akimueleza
jambo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
wakati alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za Makazi katika Manispaa
ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Meneja Mawasiliano
wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa
Khalfan Haule (kulia) wakati alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za
Makazi katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa jana. Kulia kwa Naibu Waziri
ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya.(PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANMM RUKWA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kuhakikisha inakamilisha mradi wake wa ujenzi wa nyumba za Makazi za Jangwani
katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa katika kipindi cha mwaka huu wa
fedha 2019/2020.
Akizungumza wakati
akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba hizo za makazi wenye jumla ya
nyumba ishirini za ghorofa moja jana katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa
Rukwa Naibu Waziri Mabula alisema mradi huo lazima ukamilishwe mapema kwa kuwa
fedha iliyotumika ni nyingi.
Kauli hiyo ya Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafuatia kuelezwa na Mkuu wa
mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo kuwa mradi huo umekuwa ukimsumbua kutokana na
kuchukua muda mrefu bila kukamilika na hivyo kuufanya mkoa kutojua hatma yake
wakati uhitaji wa nyumba za kupanga katika manispaa ya Sumbawanga ni mkubwa.
‘’ Naungana na RC kuwa
mradi huu umechukua muda mrefu hivyo ni lazima uishe katika mwaka huu wa fedha
wa kiserikali na April mwaka huu 2020 narudi hapa Sumbawanga’’ alisema Dkt
Mabula.
Kwa mujibu wa Meneja
Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya, mradi huo wa
ujenzi wa nyumba za Makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga ulianza mwezi
Juni 2014 na ulisimama kupisha uchunguzi baada ya kuwepo tuhuma za ubadhilifu kwenye
mradi huo.
Hata hivyo, Saguya
alisema kiasi cha shilingi milioni 366.2 kinahitahika kumalizia mradi huo na
tayari Shirika lake limejipanga na maandalizi kwa ajili ya ukamilishaji mradi yamekamilika
na muda wowote umaliziaji nyumba hizo utaanza.
Mradi huo wa Nyumba za
Makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa ambao nyumba moja
ilishanunuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF) zikikikamilika
zitapangishwa na zitaweza kuliingizia Shirika la Nyumba la Taifa kiasi cha
shilingi 5,400,000 kila mwezi.
No comments:
Post a Comment