Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) akishiriki
ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari Uchile iliyopo kata ya
Kasanzama, Wilaya ya Sumbawanga wakati alipokwenda kutembelea kujionea
miundombinu ya shyule hiyo ilivyo pamoja na hali ya kuripoti kwa
wanafunzi wa shule hiyo.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku
tano kwa wazazi kuwaandikisha watoto waliofikisha umri wa kuanza shule pamoja na
kuwafikisha shuleni wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambao
kwa mwaka 2020 wanafunzi 16,062 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika
mkoa lakini hadi kufikia tarehe 24.1.2020 ni wanafunzi 11,149 pekee wameripoti
ambao ni sawa na asilimia 69.41.
Aidha, katika kuhakikisha asilimia 100 inafikiwa amewaagiza
watendaji wa Kata na vijiji mkoani humo kuwakamata na kuwashitaki kwa sheria ya
mtoto ya mwaka 2009 wazazi wasiofanya hivyo na kuongeza kuwa sheria hiyo ya
mtoto iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inatamka wazi haki ya mtoto ikiwemo
haki ya kupata elimu na kwa mzazi kutofanya hivyo ni kosa na adhabu yake ni
kulipishwa faini au kufungwa jela ama vyote viwili kwa pamoja.
“Mimi natoa siku tano za wiki hii kwa wazazi wote ambao
wana watoto hawajaenda shule mpaka sasa hivi iwe ni wa darasa la kwanza, wawe
ni “form one” (kidato cha kwanza) baada ya siku hizi tano wakamatwe wafikishwe
mahakamani hatutaki mchezo kwenye elimu, huyu mtoto ukimchezea chezea hivi huyu
huyu ndio atatusumbua, kwasababu akitoroka shule anakimbia yamesmshinda ndio
huyo anakwenda mitaani, unadhani watoto wa mitaani wanatoka wapi si wameshindwa
shule huku, si wazaqzi wameshindwa kuwalea, wakamatwe wazazi wanashindwa
kuwalea watoto wao wafikishwe mahakamani, watendaji wa vijiji watendaji wa kata
kamateni wazazi hao” Alisisitiza.
Ameyasema hayo leo tarehe 27.1.2020 katika kikao kazi
kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji na kata za Halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo walioongozwa na makamu
Mwenyekiti wa halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akianza ziara
yake ya siku nne ya kukagua idadi ya wanafunzi walioripoti shule pamoja na
mindombinu iliyopo.
Mh. Wangabo amesema kuwa mkoa kufanya vibaya kwenye
elimu kunachangiwa na kuchelewa kupeleka watoto shule na kuongeza kuwa endapo
tathmini inafanyika kwa wale wanaofanya vibaya kwenye mitihani yao utagundua ni
wale wanaochelewa kufika shule na
kutahadharisha kuwa wanafunzi wa kidato
cha kwanza wapo katika kipindi cha mabadiliko kutoka kwenye ufundishwaji wa Kiswahili
kwenda kwenye ufundishwaji wa kiingereza hivyo ni muhimu kwao kuwahi shuleni.
“Anatoka mazingira ya shule ya msingi anaingia ya
sekondari , inapaswa mwanafunzi wa “form one” aanze mapema hata kabla ya shule
kufunguliwa ili aaanze kuzoea zoea yale mazingira lakini hajafika mapema, shule
imefunguliwa hayupo, mwezi mzima unapita hayupo shuleni , huyu hata “form two”
unategemea atafaulu kweli?” Alihoji.
Halikadhalika, Mh. Wangabo amewataka watendaji hao
kushirikiana na wenyeviti wa vijiji kuitisha mikutano ya vijiji na kuwaelimisha
wazazi juu ya umuhimu kumuwahisha mtoto
mapema shuleni huku wakiwabainishia faida na hasara za kutofanya hivyo na
kuwaeleza juu ya umuhimu wa kusomesha watoto kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa
ujumla.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni 4,394 huku walioripoti ni wanafunzi
2,973 ambao ni sawa na asilimia 67.7 huku wakihitaji madarasa 18 ambapo
madarasa 15 tayari yamefikia usawa wa linta huku Mh Wangabo akitoa
ahadi ya kuchangia mifuko
ya saruji 150 ili kuwezesha kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
No comments:
Post a Comment