Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea hundi ya kiasi cha Sh. Milioni 300,
kutoka kwa Mkuu wa Masoko Kiwanda cha Simenti Mbeya Bw. Mark Chilambe. Wa pili
kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Hazina, Bw.
Athumani Mbuttuka, wa kwanza kulia ni Naibu Katibu wa Wizara hiyo Bi. Marry
Maganga wakati wa halfa ya kupokea gawio jijini Dodoma.
(Picha na: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango).
Na Mwandishi Wetu
Wenyeviti,
Wakurugenzi wa Taasisi, Mashirika na Kampuni wamesalimika na panga la Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango baada ya kutoa gawio na michango kiasi cha
shilingi bilioni 25.12, katika kipindi cha siku 60 za utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la kuzitaka Taasisi, Mashirika na
Kampuni ambazo hazijatoa gawio kwa Serikali, kuwasilisha gawio na michango ya
huduma za Jamii.
Hayo yamedhihirishwa Jijini
Dodoma katika hafla ya kukamilisha agizo hilo la kupokea gawio kutoka katika
Mashirika, Taasisi, Wakala na Kampuni zinazomilikiwa na Serikali ambazo
hazikuwa zimefanya hivyo hapo awali.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango alisema kuwa
ameridhishwa na utekelezaji wa agizo hilo ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa tarehe 24
Novemba, 2019 na kupokea Gawio, Michango ya asilimia 15 na Michango ya Huduma
za Jamii kutoka Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki
hisa chache.
“Naomba tuungane kumshukuru
Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uongozi wake uliopelekea
Mashirika, Taasisi, Wakala na Kampuni zote ambazo Serikali ina hisa kutoa gawio,
michango ya asilimia 15 na michango ya huduma za jamii. Kama kawaida yake, Mhe.
Rais amevunja rekodi, maana haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu“, alisema Dkt.Mpango.
Alisema agizo limetekelezwa kwa asilimia
100 katika
kipindi kifupi na kuahidi kuwa fedha zote zilizokusanywa Serikali itazitumia vizuri kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Aidha, Dkt. Mpango aliwaagiza Wenyeviti wa Bodi na
Watendaji Wakuu wote wa Taasisi
na Mashirika ya Umma, wasisubiri maelekezo ya Mhe. Rais ndio waanze
kulipa gawio na michango kwa Serikali, kila mmoja kwa wakati wake akawajibike ipasavyo kuinua utendaji kwa kulipa gawio na
michango kwa hiyari.
“Ninawakumbusha
kwa niaba ya Serikali hakikisheni mnapunguza matumizi yasiyo ya lazima katika
Mashirika/Taasisi mlizodhaminiwa kuziongoza. Sitarajii mwaka ujao kuona Taasisi ama
Mashirika ya Umma kutoa michango yao kwa
kusukumwa. Ni aibu”, alisisitiza Waziri Mpango.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Bw. Athumani
Mbuttuka alisema kuwa Mashirika nne (4) pekee ndio yameshindwa kulipa gawio na michango kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na uzalishaji, upya wa taasisi na kampuni
nyingine kurejeshwa Serikalini kutokana na Mwekezaji kutokidhi vigezo vya
mkataba wa Ubinafsishaji.
Alimpongeza Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
kwa kuwezesha kukusanywa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 25.12 katika kipindi
kifupi na kubainisha kuwa fedha hizo zikitafsiriwa kwa harakahara ziweza
kujenga wastani wa vituo vya Afya 65.
No comments:
Post a Comment