NA TIGANYA VINCENT,
TABORA
SERIKALI ya Mkoa wa
Tabora imetoa miezi miwili kwa Wahandisi kuhakikisha wamesajiliwa na kupata leseni
za uhandisi zinazotolewa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB) ili
wanapokuwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali waweze kutambulika.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifungua semina ya siku moja ya
utendaji kitaalamu katika fani ya uhandisi kwa Wahandisi wa Kanda ya Magharibi
na Ziwa.
Alisema kuwa baada ya
kipindi hicho kupita hataki kuona Mhandisi asiye na leseni ya ERB ndani ya Mkoa
wa Tabora anafanyakazi.
Mwanri alisema utaratibu
wa utoaji wa leseni ni muhimu katika kuhakikisha Wahandisi wanaosimamia miradi
wanatambulika na wako tayari katika kuhakikisha usalama wa mazingira na maisha
ya wananchi.
Alitoa wito Wahandisi
wote ambao hawasijali kuhakikisha watumia nafisi hii ambapo Bodi yao inaendelea
kuhuisha leseni ambazo muda wake umekwisha ili ziwe hai na waweze kutekeleza
majukumu yao kwa uwazi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza
kuwa waandisi wasipozingatia taaluma zao ni hatari sana kwani majengo
yataanguka, madaraja yatabomoka, miundombinu mbalimbali itakuwa hafifu isiyo na
ubora hivyo kuleta maafa na hasara kubwa kwa uchumi wa taifa.
Alisema serikali
inaendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya kimkakati na wasimamizi wa
utekelezaji wake ni waandisi hivyo wanapaswa kuzingatia miiko na maadili ya
taaluma za utendaji kazi zao.
Mapema Msajili wa Bodi ya
Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi alisema hadi kufikia sasa kuna
jumla ya Wahandisi 3,373 waliopisha na kuna 26,918 ambao wamesajiliwa
kufanyakazi nchini.
Alisema kati ya hao 2,700
sawa na asilimia 11 ni wa kike ambapo lengo la Bodi ni kufikia asilimia 50 kwa
50 ndani ya muda mfupi ujao.
Mhandisi Barozi aliongeza
Wahandisi wa kike wamekuwa waamiifu wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali
wanayopewa kusimamia na ndio maana Bodi inataka kuongeza idadi yao hapa nchini.
Katika semina hiyo jumla
ya Wahandisi 16 wameapishwa na kupatiwa leseni za Bodi.
No comments:
Post a Comment