Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 31 Januari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane Jijini Dodoma. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba
(Mb) amewahakikishia watanzania kuwa serikali imekusudia kuhakikisha kuwa
mabwawa yaliyopungua kina yanakuwa na maji na kuwa na uwezo wa kufanya kazi.
Mhe Mgumba ameyasema hayo tarehe 31 Januari
2020 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Chilonwa Mhe Joel Mwaka
Makanyaga ambaye alitaka kufahamu serikali ina mpango gani kukabiliana na
mabwawa ya umwagiliaji yaliyopungua kina katika kijiji cha Buigiri,
Chalinze na Izava.
Amesema kuwa Bwawa la Buigiri ambalo
lipo katika Kata ya Buigiri lilijengwa mwaka 1960 likiwa na uwezo wa kumwagilia
hekta 40 na kunyweshea mifugo. Bwawa hilo limekuwa likijaa mchanga na tope
kutokana na mafuriko na hivyo kupungua kwa kina cha maji.
Pamoja na Serikali kukarabati bwawa
hilo katika kipindi cha mwaka 2005 na mwaka 2009 kwa kuongeza kina kwa mita
moja bado bwawa hilo liliendelea kujaa mchanga na tope kutokana na shughuli za
kibinadamu zinazofanyika juu ya bwawa na kusababisha mchanga natope kujaa
bwawani.
Mhe Mgumba amesema kuwa Tathmini
iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha kuwa bwawa hilo linahitaji ukarabati wa
sehemu ya kutoroshea maji (spillway)
na kunyanyua tuta ili kuongeza kina kwa gharama ya Shilingi milioni 475.
Amesema kuwa Bwawa
la Ikowa lililopo katika kijiji cha Chalinze na Ikowa lilijengwa mwaka 1959 kwa
ajili ya kupata maji ya mifugo na kumwagilia jumla ya hekta 96 kati ya hekta 220
katika skimu ya Chalinze.
Kutokana na
mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, bwawa
hilo limekuwa likijaa mchanga na tope kila msimu wa mvua na hivyo
kusababisha athari katika Tuta na
kupungua kwa kina cha maji katika bwawa hilo.
Bwawa la Izava lilijengwa miaka ya 1972/73 kwa ajili
ya mifugo na kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na changamoto ya kujaa mchanga na
matope bwawa hilo liliendelea kutoa huduma kwa wananchi hadi mwaka 2015 ambapo kupitia
mradi wa TASAF lilikarabatiwa na wananchi
kupitia utaratibu wa kufanya kazi za kujitolea na kutumia kiasi cha Shilingi
7,418,000/= kuwalipa wananchi hao. Mwaka 2017/18 wakati wa mvua za msimu kingo
za bwawa hilo zilibomoka na hivyo kushindwa kutunza maji kwa ajili ya kilimo.
Kadhalika, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba, akijibu swali
la Mbunge wa Solwa Mhe Ahmed Ally Salum kuhusu Bwawa la Ishololo katika Kata ya
Usule na Misengwa ni mabwawa ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa muda mrefu
sasa nlakini wizara imeomba maombi maalum ili kupata fedha za kukamilisha
miradi hiyo miwili.
Amesisitiza kuwa wizara ya kilimo imejipanga kuhakikisha kuwa
inasimamia miradi ya umwagiliaji iliyoshindwa kukamilika kwa wakati kabla ya
kuanza miradi mingine mipya.
No comments:
Post a Comment