Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya Raia wa Tanzania
55 waliokuwa wamezamia nchini Afrika Kusini, wamefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kati yao 22 wamehukumiwa kutumikia
kifungo cha miezi sita gerezani baada ya kukiri kosa la kutoka nchini
bila kufuata taratibu za kisheria.
Washitakiwa
hao ni Mzuzuri Mohammed, Mohammed Said, Masoro Musa, Mneke Mehra, Kibila
Husein, Ali Hassan, Jamalino Rashid, Abdul Nassoro, Waziru Adam na Said
Salum, Chuwa Sadick, Salum Kasimum, Macalot Alex, Kayenga Winston,
Idali Charles, Ibrahim Mohammed, Jafari Zebra, Omane Fizo, Mbona Edson,
Ulembo Azide, Fizo Charles na Mnangwa Rajab.
Akiwasomea
adhabu, Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo, amesema anawatia hatiani
washtakiwa hao kwa kuondoka nchini bila kufuata sheria za uhamiaji na
kwamba akiwaangalia wote ni vijana wenye nguvu na ambao wangeweza
kufanya kazi za kujenga Taifa badala ya kutorokea nje ya nchi ambako
wanakuwa ni wahamiaji haramu ambao wanalitia taifa letu aibu.
Alisema
kitendo cha washtakiwa siyo kwa kwanza hapa nchini, kimekuwa
kikijirudia rudia mara kwa hivyo, wameliingizia Taifa gharama kwa kukodi
ndege ya kuweza kuwarudisha nchini wakati fedha hizo zingeweza kujengea
hospitali na kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
"Makosa
haya yamekuwa yakijirudia hivyo mahakama hii inawapa adhabu ya kifungo
cha miezi sita jela bila faini na mkafanye kazi mbalimbali
mtakazopangiwa na magereza," alisema Hakimu Mwaikambo.
Kabla
ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Shija Sitta aliiomba
mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa vijana
wengine na kudai kuwa taratibu za kusafiri nje ya nchi zipo na kwamba
hakuna msingi wa watu kwenda Afrika Kusini bila kibali kitendo ambacho
kimezalilisha taifa kwa kuonekana ni wahamiaji haramu.
Washitakiwa hao kwa nyakati tofauti waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu ili kulitumikia taifa.
Awali,
akisoma mashtka, wakili Sitta alidai washitakiwa hao walitoka nje ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na kanuni za uhamiaji namba 20
(3) (a) G.N namba 657 ya mwaka 1997 inayosomwa pamoja na kifungu namba
48 (2) ya Sheria ya Uhamiaji namba 54 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2016.
Alidai Januari 21, mwaka huu maeneo ya
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), washitakiwa hao
wakiwa raia wa Tanzania walikutwa wakiwa wametoka nje ya nchi bila
kufuata utaratibu wa kutoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa kupitia
mipaka inayojulikana.
Washitakiwa wote
wamekubali mashitaka hayo na upande wa mashtaka uliwasomea maelezo ya
awali ambapo wakili wa serikali Godfrey Ngwijo alidai tarehe
zisizofahamika walitoka Tanzania na kuingia Afrika Kusini bila kufuata
taratibu.
Ngwijo alidai katika tarehe hiyo,
washitakiwa walikamatwa nchini Afrika Kusini na kuletwa Tanzania na
kwamba walifikishwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere na kwamba walipelekwa Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam na
kuchukuliwa maelezo.
Aidha washtakiwa wengine
18, wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salim Ally na wamehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela ama kulipa faini ya sh. Elfu 50.
Washtakiwa
hao ni, Adul Zuberi, Rajab Kassim, Rashid Yasin, Mussa Twahir, Twaha
Sherif, Mbaruku Amran, Kuambiana Ally, Khaulusha Said, Ladu Mukapa,
Juma Sharan, Ramadhani Issa, Amadi Katundi, Mapunda Cosmas, Mwinshehe
Hassan, Dotto Nyungwa, Asann Mohamed, Winfred George na Tikoini.
Hata
hivyo, mahakama hawakuweza kuwasomewa washtakiwa wengine 19 mashtaka
yao hadi Januari 27, 2020 (Jumatatu) kwa sababu hakimu Augustina
Mmbando aliyepaswa kusikiliza kesi yao amepata udhuru.
No comments:
Post a Comment