HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2020

Watu 11 washikiliwa kwa hujumu mizani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia Sekta ya Ujenzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Sekta hiyo, Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo katika kikao cha Baraza la Sekta hiyo, mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi (kushoto), pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa ufunguzi wa baraza hilo, mkoani Iringa.


NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema watu 11 wameshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini kwa mahojiano baada ya kubainika kufanya vitendo viovu katika mizani  hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia Sekta ya Ujenzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Sekta hiyo, Msanifu Majengo, Elius Mwakalinga, katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza hilo lililofanyika mkoani Iringa.

Alisema pamoja na mambo mengine wizara itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wasafirishaji ambao wataokiuka sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016.

“Toka tuanze mfumo tumeshawashika watu 11 na bado tunaendelea kufuatilia ili tuwashike zaidi na hatua kali zitachukuliwa ili kukomesha vitendo vya uhujumu katika mizani”, alisisitiza Mwakalinga.

Mwakalinga alisema hatua hiyo imetokana na sekta hiyo kuanzisha utaratibu wa kufuatilia utendaji kazi wa mizani kwa saa ishirini na nne kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kamera za CCTV kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa mizani na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Aidha, alifafanua kuwa sekta imeanza mchakato wa ununuzi wa gari kwa ajili ya mfumo wa kusimamia miundombinu ya barabara kwa ufanisi, weledi na kwa gharama nafuu ikiwa na lengo la kuhakikisha kazi za ukaguzi wa barabara zinafanywa kwa ufanisi.

“Gari hilo litakuwa la kisasa na lenye mionzi itakayowezesha kukagua mtandao wote wa barabara hapa nchini ndani ya mwezi mmoja na kutoa majibu ya ubora na mapungufu ya barabara kuanzia hatua za awali za ujenzi hadi mradi utakapokamilika”, alisema Mwakalinga.
Aidha, alisema sekta hiyo imekwisha peleka wataalamu 33 kwenye miradi mbalimbali nchini ili kuleta mapinduzi katika eneo hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, ameipongeza sekta hiyo kwa kuandaa baraza hilo na mikakati mbalimbali ya kimaendeleo ambayo ina lengo la kukuza uchumi wa nchi.
“Nichukue fursa hii kuipongeza sekta hii kwa kuandaa baraza hili na mikakati ya kiutekelezaji ambayo mmejiwekea, naamini kupiti mipango yenu nchi hii itapata wataalamu wengi zaidi ambao wataweza kusaidia kuleta maendeleo ya Taifa hili”, alisema Hapi.
Ameipongeza sekta hiyo kwa kuchagua mkoa huo kwa kufanya baraza hilo na kuwaalika kutembelea vivutio vilivyopo katika mkoa wake ili kuhamasisha utalii wa ndani na kuongeza pato la Taifa.
Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi la siku mbili ambalo lina wajumbe zaidi ya 100 limekutana kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa sekta, mafanikio pamoja na changamoto za sekta hiyo ili kufikia maamuzi yanayohusu sekta ya ujenzi na taasisi zake.

No comments:

Post a Comment

Pages