HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 18, 2020

Vitabu mil.5.6 vya shule za awali hadi sekondari za serikali kugaiwa

Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk. Annet Komba, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa usamabazaji wa vitabu vya shule za awali hadi sekondari.
 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa usamabazaji wa vitabu vya shule za awali hadi sekondari kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk. Annet Komba. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo TET, Fika Mwakabungu.
   
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa usamabazaji wa vitabu vya shule za awali hadi sekondari. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk. Annet Komba na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo TET, Fika Mwakabungu

Na Irene Mark

KATIKA kuhakikisha kwamba Serikali ya awamu ya tano inaboresha sekta ya elimu, leo Januari 17,2020 Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imechapisha na kuanza kusambaza vitabu zaidi ya milioni 5.6 kwa shule za msingi, sekondari na viongozi wa walimu.

Usamabazaji wa vitabu hivyo vya masomo mbalimbali vilivyoandaliwa na TET utafanyika kwenye Halmashauri za mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo leo vimeanza kugaiwa mkoani Ruvuma.

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa kuanza usamabazaji wa vitabu hivyo leo jiji Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk. Annet Komba alisema lengo la uandaaji wa vitabu hivyo ni kuhakikisha Serikali inatoa elimu  bure na bora kwa
jamii.

Alisema kati ya vitabu hivyo vitabu vya kiada kwa darasa la sita ni 2,692,155 na viongozi vya walimu wa madarasa hayo ni 224,000.

Kwa mujibu wa Dk. Komba, vitabu vya elimu ya awali ni 719, 905 wakati darasa la kwanza na la pili wakipata vitabu 500,000 na viongozi vya mwalimu wa madarasa hayo ni 400,000 huku akisisitiza kwamba ngazi ya sekondari vitabu vitakavyosambazwa ni 690,000.

Alisema vitabu vya darasa la sita kuwa ni Kiingereza, Uraia na Maadili, Hisabati, Maarifa ya Jamii, Stadi za Kazi, Kiswahili, Kifaransa na Sayansi na Teknolojia.

"Vitabu hivi kwa upande wa darasa la sita na sekondari vitagawiwa kwa uwiano wa wanafunzi watatu kitabu kimoja na elimu ya awali, la kwanza na la pili vimeongezwa kwa uwiano wa kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja," alisema Dk. Komba.

Alifafanua kuwa vitabu aina 15  ni vya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne ambavyo ni Baiolojia, Kemia, Fizikia, Hisabati, Jiografia, Historia na Kiswahili.


Dk Komba alisema uandishi wa vitabu vya hivyo ulianza  Februari, 2019 kwa ushirikiano na wataalamu wabobezi wa vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya ualimu, shule za msingi, wataalamu wastaafu na wataalamu kutoka mashirika binafsi.

"Hawa wote walitumika katika hatua mbalimbali kama kuandika andiko la awali, kufanya uhariri wa maudhui na kufanya uhariri wa lugha,"

Akishuhudia uzinduzi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo aliipongeza TET kwa  kazi nzuri ya uchapishaji vitabu hivyo na kusisitiza kuwa sasa wanafunzi wote wa watarudi kwenye shule za serikali.

"Serikali ina fungu la kutosha elimu bure ikiwemo uandishi wa vitabu. Nawaomba watendaji watumie vitabu hivi kufundishia na si kuviweka stoo," alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Pages