Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akisikiliza na kuchukua maoni ya mwananchi wa Wilaya ya Sikonge, Salum Mohammed, alipokuwa akikagua hatua za maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa kilometa 117 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora leo. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI
imeagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) katika mikoa yote kusimamia
wakandarasi waliopo kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa
kwa kuzingatia ubora katika matabaka yote ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa
makalvati yenye uimara ili kulinda barabara ziweze kuishi miaka mingi
zaidi.
Aidha, imesisitiza
kuwa inataka kuona fedha zinazotumika katika miradi hiyo ikiendana na
ubora ili kuipunguzia gharama kubwa za matengenezo ya barabara hasa
vipindi hivi vya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati wa ziara
yake ya kikazi mkoani Tabora ya kukagua athari kubwa zilizotokana na
mvua kubwa kunyesha katika miundombinu ya barabara iliyokamilika na ile
inayoendelea kutekelezwa ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi
wa barabara ya Usesula - Komanga yenye urefu wa kilometa 117
inayojengwa kwa kiwango cha lami.
"Nimefurahishwa
na mradi huu kwani mwaka jana nilipita hapa kwenye barabara za mchepuo
lakini leo nimepita kwenye lami imara", alisema Naibu Waziri Kwandikwa.
Alieleza
kuwa ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika mapema utaufungua mkoa wa
Tabora na Katavi kwa kiwango cha lami na hivyo kufanya Sera ya Awamu ya
Tano ya kuunganisha mkoa kwa mkoa inaendelea kutimia.
Kwandikwa,
alisema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaojengwa na mkandarasi
Jiangxi Geo - Engineering umefikia asilimia 39.7 huku kilometa 43.2
tayari zimeshawekwa lami.
Naibu
Waziri huyo alisema kuwa wao kama Wizara wako tayari kutoa ushirikiano
kwa mkandarasi na TANROADS ili mradi huu ukamilike kwa wakati.
Alisisitiza
kuwa mbali na kazi nzuri zinazofanywa na TANROADS kwa ajili ya
usimamizi wa miradi mikubwa Serikali inaendeelea kutoa fedha kwa ajili
ya kufungua mikoa yote ya nyanda za magharibi kwa mtandao wa lami.
"TANROADS
msimamie mkandarasi huyu tunataka kazi ziende kwa kasi lakini
zishikamane na ubora zaidi", alisisitiza Naibu Waziri huyo.
Awali
akitoa taarifa ya mradi kwa Naibu Waziri huyo Kaimu Meneja wa TANROADS,
mkoa wa Tabora Mhandisi Raphael Mlimaji, amemuhakikishia Naibu Waziri
huyo kumsimamia mkandarasi kwa karibu na kuhakikisha hakuna dosari
zozote zitakazoweza kujitokeza siku za usoni.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatumia aina ya lami (superpaved) ambayo
ni imara sana na yenye kumudu vipindi vya baridi na joto.
No comments:
Post a Comment