Na Tiganya Vincent
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri
ya Wilaya ya Tabora(Uyui) limetakiwa kuwachukulia hatua watendaji waliopewa
jukumu la kukusanya mapato ya ndani ambao utumiaji fedha hizo kinyume cha
Sheria na taratibu na kusababisha kuzalisha hoja za kikaguzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana
na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Tabora anayeshughulikia Mamlaka ya Serikali za Mitaa Emmanuel Kuboja wakati
wa mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.
Alisema kuwa pindi
inapobainiki mtumishi aliyepewa kukusanya mapato ya Halmashauri ametumia fedha
alizokusanya kinyume cha taratibu achukuliwe hatua mapema badala la kumpa muda
mrefu kurejesha fedha.
“Tusiwaone huruma
watumishi waliopewa POS kwa ajili ya kukusanya mapato badala yake fedha
hawapeleki Benki na kuishia mifukoni mwao…sioni sababu ya kuwaambia ndani ya
mwezi warudishe fedha …wanatakiwa kurudisha palapale” alisisitiza.
Kuboja aliitaka
Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Tabora (uyui) kutotumia fedha za mapato
ya ndani bila utaratibu wa kuyaingizwa Benki.
Alisema ni marufuku mkusanyaji kuendelea kukusanya nyumbani kwake ni lazima kila zinapokusanywa zipelekwe kwanza katika Benki
husika ndio utaratibu wa matumizi halali upangwe.
“ Matumizi ya fedha
mbichi ni hatari …zitasababisha upotevu wa mapato ya umma na kupelekea
Halmashauri kuzalisha hoja ambazo zinawatia doa” alionya.
Aidha Katibu huyo
Msaidizi wa Mkoa alimtaka Mkurugenzi Mtendaji kuchukua hatua haraka anapobaini
mapungufu kwa wakusanyaji mapato ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya
Tano.
No comments:
Post a Comment