HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 04, 2020

Waziri Kamwelwe aagiza MAB kutanguliza uzalendo mbele

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (mbele) mwishoni mwa wiki akiongea na Walioteuliwa kuunda Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), pamoja na Menejimenti ya TAA wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo katika Jengo la TPA (One Stop Centre) jijini Dar es Salaam.
Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (mwenye suti ya maji ya bahari), na Mwenyekiti, Dkt Masatu Chiguma na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki kwenye Jengo la TPA.

 
Na Bahati Mollel, TAA

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe ameiasa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), kutanguliza Utaifa na Uzalendo mbele katika majukumu yao.

Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki katika halfa ya uzinduzi wa Bodi hiyo, ambao umefanyika kwenye Jengo la Bandari nchini (TPA One Stop Centre) lililopo jijini Dar es Salaam.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa kwamba, nafasi hizi mlizopewa ni kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa huku mkitanguliza maslahi mapana ya taifa na uzalendo mbele”. Amesema Waziri
Kamwelwe

Pia Waziri Kamwelwe ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha inashirikiana bega kwa bega na menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na taasisi za serikali hususan Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika
ujenzi wa viwanja vingi zaidi ya wanavyovisimamia 58 kwa lengo ya kuviongeza, ili ndege za Shirika la ndege Tanzania (ATCL) na mashirika mengine yaweze kupanua wigo wa safari.

Halikadhalika amesema ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege ukaimarishwe, ingawa bado kunachangamoto ya kukosekana kwa uzio wa ndani na nje ya viwanja vya ndege, ambapo pia suala la ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona ulioanzia nchini China lipewe kipaumbele kwa kuzingatiwa
maslahi mapana ya Taifa yazingatiwe.

“Hili la ugonjwa wa Corona liangaliwe kwa ukaribu zaidi ili viwanja vya ndege visiwe ndio njia ya kuingiza ugonjwa huu, pia usalama wa watendajikazi uangaliwe pia,” amesema na kuongeza.

“... Vilevile mkahakikishe kuwepo na usimamizi mzuri wa wa ardhi na miundombinu ya viwanja vyetu ikiwemo Jengo la Tatu la abiria –JNIA na utoaji wa huduma bora zaidi kwa wateja, ukiangalia kwa sasa ni viwanja vichache tu ndio vina hati na hili sio jambo jema, hakikisheni viwanja vyote
vinapimwa na hati kupatikana, kwani itasaidia kuongeza uhalali na kuongeza mapato ya TAA kwa kutumia ardhi hiyo,” amesema Waziri Kamwelwe.

Pia ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha TAA inapata “control number” ili malipo mbalimbali yatafanyika kupitia huko, ambapo pia ameitaka kubuni njia mbalimbali za kuendesha viwanja vya ndege kibiashara, wakati sasa suala la
TAA kuwa Mamlaka zaidi badala ya sasa kuwa Wakala pamoja na kwamba lipo chini ya Wizara linahitaji msukumo wa Bodi hiyo.

Hatahivyo, Waziri Kamwelwe amesema pamoja na TAA kuwa na mafanikio bado inakabiliwa na changamoto za kushindwa kuboresha miundombinu mbalimbali iliyopo viwanjani.

Bodi hiyo inaundwa na Mwenyekiti Dkt. Masatu Chiguma na wajumbe ni Mhandisi Ven Kayamba, Dkt. Paschal Mugabe, Mhandisi Daniel Kiunsi, Mhandisi Christopher Mukoma na Alex Haraba.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Mshauri, Julius Ndyamukama amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikikua tangu kuanzishwa kwake hadi sasa, na kutolea mfano wa mapato kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 6.3 hadi kufikia Bilioni 105.2 kwa mwaka, ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia
1,570.

Pia amesema Mamlaka ilianza na ikiwa na miruko na mituo ya ndege 62,221 kwa mwaka na sasa imefikia 146,593 kwa mwaka ni sawa na ongezeko la
asilimia 135.6.

Kwa upande wa abiria, amesema ilianza ikiwa na idadi ya abiria 846,906 kwa mwaka na sasa imefikia 3,473,658 kwa mwaka ikiwa ni sawa na ongezeko la
asilimia 310.

Naye Mwenyekiti wa MAB, Dkt. Masatu Chiguma, alimuahidi Waziri kuwa atafanya kazi bega kwa bega na TAA, ili kufanikisha malengo yalilowekwa.

No comments:

Post a Comment

Pages