Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli akiongoza Kikao cha Usalama na Maadili kilichofanyika katika Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, jijini Dar es Salaam leo Februari 12, 2020. (Picha na Ikulu).
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
TAARIFA
KWA UMMA
KIKAO
CHA KAMATI KUU MAALUM YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
_______________
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba
12 Februari 2020
Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Kamati Kuu
(KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imeketi leo Jijini Dar es Salaam chini
ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kikao cha Kamati Kuu
(KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kimeketi pamoja na mambo mengine kimepokea
taarifa zifuatazo; -
Maandalizi ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 –
2030 na Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Kamati Kuu imepokea
taarifa ya Maendeleo ya Uandishi wa Waraka huu muhimu wa Kisera na kujiridhisha
na kazi nzuri ambayo imekwisha kufanyika mpaka ngazi ya Rasimu. Kamati Kuu pia
imepitia zoezi la uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020
na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya
kukamilisha uandishi wake ili vikao vya Chama vifanye uamuzi na kupitisha.
Maombi ya Kujiunga na uanachama wa CCM kutoka kwa Ndg.
Fredrick Tluway Sumaye
Kamati Kuu (KK) ya
Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imepokea taarifa ya Maombi ya kujiunga na CCM
kutoka kwa Ndg. Fredrick Tluway Sumaye Waziri Mkuu Mstaafu na kupongeza kazi
nzuri inayofanywa na Chama na Serikali ambayo imekiletea Chama heshima kubwa na
ukubalifu kwa umma wa wananchi, wanachama na viongozi wa vyama vingine vya
siasa. Kikao kimempongeza Ndg. Sumaye kwa uamuzi wake, kimeelekeza utaratibu wa
kujiunga rasmi katika Chama ufuatwe kwa mujibu wa Katiba ya CCM.
Taarifa ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu
Kamati Kuu imepokea
Taarifa ya Awali kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili juu ya Utekelezaji wa
Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) katika Kikao chake cha Mwezi Disemba
2019 Jijini Mwanza kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama watatu, Ndg. Yusuph
Makamba, Ndg. Abdulrahman Kinana na Ndg. Benard Membe ambao wote wameshafika
mbele ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu inayoongozwa na Mzee Philip
Mangula, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Kamati Kuu imetoa siku saba
kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama
hawa watatu na kuiwasilisha katika Vikao husika.
KIDUMU
CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI
ZINGATIO: Video zimeshatumwa kwa vyombo vya habari
No comments:
Post a Comment