HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2020

TMA yataja sababu za joto kuzidi

Na Irene Mark
KUKOSEKANA kwa wingu juu ya anga na uwepo wa jua la utosi kwenye anga ya nchi ni sababu ya kuongezeka kwa joto hadi nyuzi joto 36 katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi.

Sababu za ongezeko la joto kwa siku tatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Zanzibar, zilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, Dar es Salaam jana wakati wa semina kwa wanahabari kuhusu maandalizi ya utabiri wa mvua za masika zitakazoanza Machi mwaka huu.

Alisema kuanzia Februari 9 hadi 11 hali ya joto kwa mikoa tajwa ilikuwa kati ya sentigredi 32.5 hadi 36 hali iliyosababisha kuwepo kwa sintofahamu kwa jamii.

"Dar es Salaam joto lilianzia nyuzi joto 33.3 mpaka 33.9 na wastani wake ulikuwa ni nyuzi joto 32.6 huku kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Morogoro nyuzi joto ilifika 34.2.

"Zanzibar ilisoma nyuzi joto 34.2 wakati matarajio yalikuwa nyuzi joto 33 na kule  Tanga nyuzi joto ilikuwa juu mpaka kufikia nyuzi joto 36 wakati matarajio yalikuwa nyuzi joto 32.8.

"...Lakini hatutegemei tena hali hiyo sababu ilileta unyevu kwenye anga nao umejikusanya na kutengeneza wingu litakalosababisha mvua kidogo kwenye baadhi ya maeneo yaliyokuwa na joto kali," alisema Dk. Kijazi.

Alisema hali hiyo haitaendelea sababu hali ya joto inapokuwa kubwa hutengeneza unyevunyevu angani na kuunda mawingu ya mvua nyepesi za vipindi vifupi.

Katika hatua nyingine TMA leo inatarajia kutoa utabiri wa mvua za masika zitakazoanza Machi, Aprili na kuishia Mei (MAM), zitakazonyesha kwenye mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka.

Mamlaka hiyo pia imewapa pole wananchi wote waliopata maafa kutokana na mvua zilizonyeesha kwenye mikoa mbalimbali huku ikiwasisirizia wananchi kuchukua tahadhari za hali ya hewa zinazotolewa Na TMA.

No comments:

Post a Comment

Pages