HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2020

TMDA wapongeza usajili wa maduka ya dawa muhimu za binadamu Njombe

Na Amiri kilagalila-Njombe
Licha ya uwepo wa changamoto katika utoaji na utekekelezaji wa huduma za afya nchini,taarifa ya mamlaka ya dawa na vifaa tiba TMDA kanda ya nyanda za juu kusini inaonyesha utekelezaji mzuri katika usajili wa maduka ya dawa za binadamu mkoani Njombe huku moja pekee likibainika kuto kuwa na usajili.
Taarifa ya matokeo ya ukaguzi  wa mwezi wa 7 mpaka wa 12 mwaka 2019 iliyosomwa katika kikao cha kawaida cha TMDA na wataalamu wa afya wa halmashauri za mkoa wa Njombe katika ukumbi wa chuo cha afya Kibena, kwa lengo la kuwaongezea uzoefu,inaonesha maduka matatu huku moja likiwa ni la dawa za binadamu na mawili ni dawa za mifugo hayakuwa na usajili pamoja na vibali vya kuendesha biashara huku wamiliki wakiagizwa kuomba usajili wa vibali ndani ya siku 14.
Aidha Idadi ya majengo ya afya yaliyokaguliwa katika kipindi hicho,kanda ilikagua jumla ya majengo 128 ikiwa hospitali 12,vituo vya afya 13,zahanati 4,famasi 9,maduka ya dawa muhimu 70,maduka ya dawa za mifugo 19 na maabara 1.
Anitha Mshighati ni kaimu meneja wa TMDA  kanda ya nyanda za juu kusini,amasema wataendelea kukumbushana na kutoa elimu ili kuepusha ukiukwaji katika utoaji huduma.
“Tunataka kuhakikisha vile vitu ambavyo tumevisajili vinaendelea kuwepo sokoni na katika ubora ule ule maana sio kila wakati wakaguzi wanakuwepo wakati wa uhishaji wa bidhaa,kwa hiyo tunatakiwa kuhakikisha ubora tulioukubali unaendelea kuwepo katika nchi yetu”alisema Anitha Mshighati
Mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt.Bumi Mwamasage amesema ukaguzi hufanyika kila robo ya mwaka katika maduka yote ya dawa mkoani Njombe licha ya kuwepo kwa changamoto za ukiukwaji wa sheria huku hatua za kisheria zikiendelea kuchukuliwa kwa wanaobainika.
Katalina Revocati ni katibu tawala wa mkoa wa Njombe,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho,ametoa rai kwa wakurugenzi wa halmashauri zote kuendelea kutekeleza majukumu ya udhibiti wa bidhaa za afya ili kulinda afya ya jamii.
“kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikijitokeza ambazo sisi sote tunatakiwa kuwa walinzi maswala haya ni kama vile halmashauri kuto kufanya kaguzi za mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma za afya na maduka ya dawa,kufuatilia dawa na vifaa tiba,hali hiyo inasababisha baadhi ya maduka na vituo vya afya kuendelea kuhifadhi dawa katika mazingira yasiyofaa hivyo kuhatarisha ubora wake”alisema Katalina Revocati
Baadhi ya washiriki katika kikao hicho wamekiri kupokea mafunzo na kwenda kuyatumia kikamilifu ili kuendelea kuboresha huduma ya afya kwa jamii.
  Kaimu Meneja wa TMDA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighatim, akiendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu/watendaji wa afya wa halmashauri za mkoa wa Njombe katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha afya Kibena mjini Njombe mkoani humo.
  Baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa makini kusikiliza,wakati wa kikao cha afya kilichofanyika mjini Njombe.
 Katalina Revocat, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, aliyekuwa mgeni rasmi akitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha wataalamu wa afya na TMDA kilichofanyika katika ukumbi wa chuo cha afya kibena.
Kaimu meneja wa TMDA,  Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati, wakati alipokuwa akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari
 Dkt. Bumi Mwamasage, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, akizunguzmza na waandishi wa habari mara baada ya hotuba ya mgeni rasmi iliyotolewa kwa wataalamu wa afya na mamlaka ya dawa na vifaa tiba kanda ya nyanda za juu kusini.

No comments:

Post a Comment

Pages