Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akizungumza na
wananchi wa Mabwepande waliofika ofisni kwake Dar es Salaam kwa ajili ya
kutatua mgogoro wa ardhi kupitia program ya Funguka kwa Waziri jana tarehe 23 Februari
2020.
Sehemu ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam waliojitokeza
kuonana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi William Lukuvi kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa migogoro yao kupitia
program ya Funguka kwa Waziri jana tarehe 23 Februari 2020. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepongezwa na wananchi wa mkoa wa Dar es
Salaam kwa uamuzi wake wa kukutana nao na kutatua migogoro ya ardhi 628 katika
mkoa huo katika kipindi cha siku tano kupitia progaramu ya Funguka kwa Waziri
hadi saa nne usiku.
Lukuvi alihitimisha
programu ya Funguka kwa Waziri kwa kukutana na wananchi wa Manispaa ya
Kinondoni jana tarehe 22 Februari kwa kusikiliza na kutatua kero, malalamiko na
migogoro mia tatu (300) iliyomfikisha saa 4:22 usiku.
Awali, Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikutana na wananchi wa Manispaa za Ilala ambapo
alishughulikia migogoro 122, Ubungo 75, Kigamboni migogoro 65 na Manispaa ya
Temeke migogoro 66 na kufanya jumla ya migogoro aliyoishughulikia kwa siku zote
tano kufikia 628.
Kati ya Wananchi
aliokutana nao tangu kuanza kwa program hiyo siku ya jumanne tarehe 18 Februari
2020, Manispaa ya Kinondoni ilioonekana kuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye malalamiko
ya ardhi ukilinganisha na Manispaa nyingine za mkoa wa Dar es Salaam.
Baadhi ya Wananchi
waliokutana na Waziri Lukuvi walionesha kufurahishwa na utaratibu wa Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kukutana na wananchi kwa nia
ya kupata suluhu ya migogoro ya ardhi iliyoelezwa kuwa imekuwa ikiwahangaisha
kwa muda mrefu bila mafanikio.
Raphael Ngowi mkazi wa
Kinondoni ambaye malalamiko yake ni kuhusiana na kiwanja chake kumilikishwa kwa
watu wawili alisema, utaratibu wa Waziri wa Ardhi kukutana moja kwa moja na
wananchi unamsaidia kupata mambo mengi kutoka kwa mhusika badala ya kusikia
kutoka kwa watendaji.
Alisema, utaratibu huo siyo
tu unasaidia wananchi wenye matatizo ama kudhulumiwa haki zao katika sekta ya
ardhi bali unatoa pia fursa kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi kubainia uzembe
wa baadhi ya watendaji wake katika maeneo yenye migogoro.
Kwa mujibu wa Ngowi,
kati ya Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano, Lukuvi amevunja rekodi kwa
kuweza kutatua matatizo ya wananchi kwa kukutana nao ana kwa ana jambo
alilolieleza kuwa limeasisiwa na Mwl. Nyerere kwa kuweka uwazi wa kushugulikia
kero.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya wenye Mashamba eneo la Mabwepande katika manispaa ya Kinondoni
Seif Maungu anayewakilisha wananchi 258 walio katika mgogoro wa kuvamiwa eneo
lao alisema, baada ya kuonana na Waziri Lukuvi sasa wamepata faraja kubwa baada
ya mateso ya takriban miaka 13.
‘’Kwa muda mrefu
tulikuwa hatupati majibu kuhusiana na mgogoro wa maeneo yetu lakini sasa baada
ya kukutana na mhe. Lukuvi tumepata faraja na Rais Magufuli amepata jembe’’
alisema Maungu.
Mkazi mwingine wa
Magomeni aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Maulid Kinyogoli aliyewasilisha
tatizo lake la kutopata Hati ya Ardhi, aliilezea program ya Funguka kwa Waziri
kuwa ni mwarobaini wa matatizo ya ardhi yanayosababishwa na watendaji wa sekta
ya ardhi wasiokuwa waaminifu.
‘’Utaratibu wa Funguka
kwa Waziri uliaonzishwa na Lukuvi kwa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi
ungekuwa ukifanywa na viongozi wengine kupitia sekta zao basi matatizo yangepungua
na hivyo kumrahisishia kazi Rais John Pombe Magufuli ya kuleta maendeleo’’
Alisema Kinyogoli.
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekuwa na utaratibu wa kukutana na
wananchi wenye malalamiko na kero za ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kwa
nia ya kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi ambapo tayari program hiyo
imeshafanyika mikoa mbalimbali ikiwemo Kilimanjaro, Tanga, Rukwa, Mbeya, Iringa,
Tabora, Kigoma, Kagera, Katavi na Lindi na kuleta mafanikio makubwa.
No comments:
Post a Comment