Na Mwandishi Wetu
MMOJA wa wapenzi
maarufu wa Yanga, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate
Mwegello (pichani), amewataka wenzake wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
wakati watakapopambana na watani wao wa jadi, Simba.
Katika mchezo huo wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ndio watakaokuwa wenyeji, wakiwa na mzuka
wa kushinda ili kuwatia presha Simba kuelekea mbio za ubingwa wa ligi
hiyo.
Ikumbukwe katika
mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye uwanja huo, timu zilitoka sare ya
mabao 2-2, wenyeji Simba wakiwa wa kwanza kupata mabao mawili, kabla ya
Yanga kusawazisha yote,
tena ndani ya dakika tatu tu.
Akizungumza na
gazeti hili jana Alhamisi, Jokate ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,
Pwani, alisema kuwa Yanga watashinda mchezo huo wa Jumapili kutokana na
ubora wa kikosi chao.
“Sina wasiwasi na
timu yangu ya Yanga, naamini itashinda tu mbele ya Simba Jumapili,
niwaombe mashabiki wa Yanga tujitokeze kwa wingi uwanjani wakiwa wamevaa
jezi za timu yetu ili
tuwape morali wachezaji wetu waweze kupambana na kupata ushindi,”
alisema Jokate aliyeitikisa fani ya urembo mwaka 2006, ikidaiwa ndiye
aliyestahili kutwaa taji la Miss Tanzania badala ya aliyepewa ushindi.
Alisema kwa kuwa
kauli mbiu ya Yanga kuelekea mchezo huo ni vaa kibingwa, basi kila
shabiki avae jezi ya mchezaji wa timu hiyo anayempenda ili kunogesha
siku hiyo wakiwa kama wenyeji
wa mchezo.
“Kwa sasa nipo
kwenye ziara huku vijijini, ila natamani iwepo uwanjani siku hiyo,
lakini hata kama nikishindwa kwenda, najua vijana wetu hawataniangusha,
tutashinda tu,” alisisitiza.
Kwa upande wake,
Meneja Masoko na Mawasiliano wa GSM Group, Matina Nkurlu, alisema
wametengeneza jezi za kutosha ili kila shabiki wa Yanga aweze kupata na
kwenda nayo uwanjani Jumapili
kushuhudia pambano hilo.
“GSM tunafahamu
mvuto wa mchezo huo, na tukiwa kama wadhamini wa Yanga na watengenezaji
rasmi wa jezi za klabu hiyo, tumehakikisha tunatengeneza jezi za kutosha
zenye ubora wa hali
ya juu ili kukidhi mahitaji ya Wanayanga.
“Jezi zimeshaanza
kuuzwa katika maeneo mbalimbali na zaidi maduka ya GSM yaliyopo Mlimani
City, Pugu Mall, Lumumba na kwingineko hivyo kila shabiki wa Yanga
ahakikishe ananunua jezi
halisi (original) ya Yanga na kuepuka kununua zile za mitaani ambazo
hazina maslahi yoyote na klabu yao,” alisema.
Alisema jezi zao
hizo zipo katika ubora wa hali ya juu unaolingana na hadhi klabu ya
Yanga. Niwaombe wanayanga wasikubali kununua jezi za mitaani ambazo ni
za wajanja wachache ambao
wamekuwa wakipiga fedha kwa kupitia nembo ya Wanajangwani hao.
No comments:
Post a Comment