HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 06, 2020

TANLAP WATOA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI WA KAGERA

Baadhi ya wananchi waliofika katika uwanja wa posta wilayani Ngara kwa ajiri ya kupata msaada wa kisheria.

 
Na Alodia Dominick, Ngara

 Mkoa wa Kagera unakabiliwa na migogoro mbalimbali ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ya ardhi, ambapo zaidi ya watu 795 sawa na asilimia 10 wamewasilisha kesi hizo kwa mwaka 2019.

Takwimu hizo zimetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao unaotoa msaada wa kisheria TANLAP, Christina Ruhinda, wakati akiwa wilayani Ngara kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji wilayani Ngara.

Christina amesema, wananchi mkoani Kagera wanakabiliwa na migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi, kesi za ubakaji, ndoa za utotoni na mimba ambapo amesema, kutokana na kesi hizo shirika la Mamas' Hope Organisation for Legal Assitance  (MHOLA) chini ya mtandao wa TANLAP limekuwa likitoa msaada wa kisheria kwa wananchi mkoani humo kwa kuwashauri namna ya kuepukana na migogoro hiyo lakini kama kuna ulazima wa kwenda mahakamani ni hatua zipi wazifuate.

Amewataja wateja waliofikiwa kwa mwaka 2019 wakihitaji msaada wa kisheria kuwa ni 7,808 kati yao 795 waliwasilisha kesi mbalimbali za ukatili wa kijinsia sawa na asilimia 10, ambapo jumla ya watu 147,000 walifikiwa kwa njia ya elimu na uhamasishaji na kutokana na sensa ya mwaka 2012 mkoa wa Kagera una watu 2.5 milioni hivyo watu waliofikiwa Kagera ni asilimia 6 hivyo bado kuna idadi kubwa ya wanakagera wanaohitaji msaada wa kisheria.

Kwa upande wa mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Marco Mtenjeri amesema kuwa, wananchi waitumie nafasi ya kupata elimu juu ya Sheria zinazohusiana na ukatili wa kijinsia ili migogoro inayowakabili iweze kupungua kama siyo kuisha kabisa.

Ameongeza kuwa, migogoro inayowakabili wananchi wa wilaya ya Ngara ni migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa na mimba za utotoni hivyo kutokana na elimu inayoendelea kutolewa ni imani yake kuwa migogoro hiyo itapungua.

Naye wakili na Mkuu wa Mhola tawi la Karagwe na Ngara Laymond Laurent ameitaja changamoto ya wananchi kutofuata taratibu wanazoelekezwa na hivyo kutaka yatolewe maamuzi kama wao wanavyotaka na kuwa kama wataona hawajaridhika na maamuzi ya mahakama wakate rufaa.

No comments:

Post a Comment

Pages