WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili
kuwahudumia watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa kali ya
mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na amesema
ameridhishwa na maandalizi.
Aliyasema
hayo jana (Jumamosi, Machi 28, 2020) wakati akizungumza na wananchi
wilayani Kibaha, Pwani baada ya kukagua hospitali ya wilaya ya Kibaha
ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu watakaogundulika kuwa na
maambukizi ya virusi vya corona.
Alisema
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabilia na
COVID-19, ambapo kwa sasa watu wote wanaoingia nchini kupitia viwanja
vya ndege, vituo vya mabasi na bandari lazima wapimwe na wakigundulika
wanamaambukizi wanawekwa kwenye maeneo maalumu kwa muda wa siku 14.
“Tunazingatia
sana wale wanaotoka kwenye nchi ambazo zimeathirika sana wakiingia hapa
Tanzania tunawazuia kwanza, tunawapima na tunafuatilia historia yake
anatoka wapi na tunaangalia katika siku 14 amepita kwenye nchi zipi.”
Waziri
Mkuu alisema wawaweka kwenye maeneo maalumu ili kuweza kuwapima kila
siku na kujirishika kama hawana maambukizi kwani mtu anaweza kupimwa leo
akaonekana yuko vizuri lakini ana maambukizi ambayo bado hayaonekani
kwenye vipimo. Kama katika kipindi cha siku 14 mtu atabainika hana
maambukizi anaruhusiwa kwenda kujiunga na familia.
Pia,
alisisitiza wananchi waendelee kufuata maelekezo yaliyotolewa na
Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzuia
mikusanyiko na kwa wale wanaosafiri kwenye usafiri wa umma wasibanane
kila mtu akae kwenye kiti.
Waziri
Mkuu alisema wananchi wanapokwenda kufuata huduma kwenye masoko
wahakikishe wanapeana nafasi baina ya mtu mmoja na mwingine na kabla
hawajaingia katika maduka wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka ili
kujikinga na maambukizi ya corona.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kuwachukulia hatua watu wote
wanaopotosha kuhusu taarifa za ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). “Aliyetangaza kuwa
shule zinafunguliwa tumeshamkamata na atachukuliwa hatua.”
Hivyo
aliwataka wananchi wajihadhari na taarifa zinazotolewa na watu ambao si
wasemaji rasmi. Alisema taarifa kuhusu virusi vya corona itatolewa na
Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
pamoja na Msemaji wa Serikali.
No comments:
Post a Comment