Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi wa Ujenzi wa
mradi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Injia Kazoba Wilson (kushoto) wakati akitoka
kukagua maendelezo ya ujenzi wa hospitali hiyo jana Musoma mkoani Mara. Wa pili
kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney.
Jengo la hospitali ya Rufaa mkoa wa
Mara lililopo eneo la Kwangwa Musoma likiwa katika hatua za ukamilishaji. (Picha na Munir Shemweta, Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM, Musoma
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameridhishwa na kasi ya
ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoko Kwangwa Musoma
unaogharimu takriban Bilioni 15.082.
Dkt Mabula aliridhishwa
na kasi ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo alipokwenda kukagua maendeleo ya
ujezi wake jana wakati akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Mara.
Alisema, ujenzi wa
mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa Mara sambamba na mikoa na nchi jirani kwa
kuwa itakuwa ikitoa huduma za kitabibu kwa wananchi wa maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibainisha kuwa, hana mashaka na Shirika la
Nyumba la Taifa katika kutekeleza mradi huo kutokana na Shirika hilo kufanya
vizuri kwenye miradi mbalimbali inayosimamia.
‘’Kwa sasa sina mashaka
na Shirika la Nyumba la Taifa katika masuala ya ujenzi kutokana na kufanya
vizuri kwenye miradi mingi ya ujenzi inayosimamia lakini kinachotakiwa hapa ni
kukamilisha ujenzi kwa wakati’’ alisema Dkt Mabula
Ameitaja baadhi ya
miradi ya ujenzi inayofanywa na NHC na kufanya vizuri kwenye maeneo mablimbali kuwa
ni ujenzi wa ofisi kumi na saba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Hospitali ya Rufaa ya Kusini iliyopo Mtwara,
Ofisi ya wilaya ya Wang’ingombe na nyumba za wakuu wa wilaya za Hai na Ulanga.
Kwa upande wake Meneja
wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mara Goodluck Thomas alisema Shirika lake
katika kutekeleza mradi huo tayari baadhi ya kazi zimekamilishwa ikiwemo jengo
la Huduma ya Mama na Mtoto, nyongeza ya ghorofa moja na kupaua, kupiga plaster
nje na ndani, maandalizi ya rangi, fremu za milango pamoja na kuweka marumaru.
Kwa mujibu wa Goodluck,
kazi zinazoendelea sasa ni uwekaji mifumo ya maji safi na maji taka, kazi ya
umeme, uwekaji mifumo ya gesi, ufungaji madirisha ya alminiuam na ukamilishaji
kazi nyingine ukiendelea na mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo umefikia asilimia
65.
Mkuu wa wilaya ya Musoma
Dkt Vincent Naano Anney alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa wakati ujenzi wa
hospitali hiyo ukiendelea kukamilishwa kuna haja kwa mamlaka husika kuanza kuangalia mahitaji ya Wataalamu na Vifaa
vinavyohitajika kwenye vitengo mbalimbali vya hospitali hiyo na kubainisha kuwa
kazi hiyo isipofanyika mapema kuna hatari ujenzi utakapokamilika hospitali hiyo
ikakosa wataalamu wa kutosha kutokana na ukubwa wake.
No comments:
Post a Comment