HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 06, 2020

WASIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOBAINIKA KUWA NA DOSARI KUCHUKULIWA HATUA

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Muganyizi Zachwa.


Na Lydia Lugakila, Kagera

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Bukoba mjini Muganyizi Zachwa katika Ziara iliyofanywa na kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya chama hicho katika kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

 Muganyizi Zachwa amesema kuwa hafurahishwi na hatoendelea kumkumbatia mtu  au kikundi cha watu wanaokwamisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hatua hiyo imekuja kutokana na kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo kubaini  baadhi ya miradi mbali mbali ya kimaendeleo kuwa ya kimashaka na kushindwa kukamilika kwa wakati huku mingine ikiwa haina ubora unaotakiwa katika kiwango cha serikali.

Zachwa amesema fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuli ya muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufanya maendeleo ya wananachi hivyo kwa Chama hicho kitachukua hatua Kali na kuwawajibisha wasimamizi wa miradi hiyo pale inapobainika miradi haisongi mbele.

"Hatuwezi kwenda namna hiyo fedha za miradi lazima zionyeshe kipi kimefanyika kwa ubora upi na kukamilika kwa wakati hayo ndo maendeleo tunayokwenda nayo" alisema Zachwa.

Mwenyekiti huyo ameeleza kukerwa na kitendo cha kuitwa kukagua miradi ya maendeleo ambayo haijakamilika na kuwaonya wasimamizi wa miradi hiyo kuwa hatokuwa tayari kukagua miradi nusu.

Katika hatua hiyo ametoa agizo kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Nyanga iliyopo katika Kata ya Nyanga manispaa ya Bukoba kukamilisha ukarabati wa vyumba vya madarasa Mara moja huku akitoa mwezi mmoja kukamilika kwa ujenzi wa shule ya sekondari Rwamishenye baada ya fedha za ujenzi wa chumba cha darasa kuisha na ujenzi kutoridhisha.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Deodatus Kinawilo amesema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi hivyo ni lazima mtu kwa nafasi yake ashiriki kujenga uchumi wa Nchi.

Hata hivyo kamati hiyo ya siasa imekagua miradi ya maendeleo ipatayo 9 katika kata 5 za manispaa ya Bukoba huku miradi miwili kugubikwa na   dosari.

No comments:

Post a Comment

Pages