Mratibu wa Kampeni wa OXFAM, Mkamiti Mgawe (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano na Maonesho ya Mabadiliko ya Tabianchi yatakayofanyika Machi 25 na 26 jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja Miradi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTEDO), Mary Swai, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Program wa Shirika lisilo la Kiserikali la FORUMCC, Angela Damas. (Picha na Suleiman Msuya).
Na Suleiman Msuya
WADAU zaidi ya 200
kutoka sekta mbalimbali nchini wanarajiwa kushiriki Mkutano Mkuu wa Sita wa
Mabadiliko ya Tabianchi na Maonesho utakaofanyika jijini Dar es Salaam,
Tanzania kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Mkutano huo unatarajia
kukutanisha wadau kutoka asasi za kiraia, waakilishi wa Serikali, wabunge,
washirikia wa maendeleo, taasisi za elimu, wabunifu, sekta binafsi, vijana,
uwakilishi wa jamii, wanawake na waandishi wa habari.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi wa Program wa Shirika lisilo la Kiserikali la FORUMCC, Angela Damas
wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa.
Damas alisema Shirika
hilo linalojihusisha na kuleta ushawishi wa kuchukua hatua
kustahimili/kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi hivyo mkutano hup
utatopa majibu sahihi ya nini kifanyike
kukabiliana na hali hiyo.
“FORUMCC na washirika
wake walikaa kuandaa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao
umekuwa ni utaratibu wa kila mwaka tangu mwaka 2015.
Mwaka huu, Mkutano Mkuu
wa Sita wa Mabadiliko ya Tabianchi na Maonesho utafanyika jijini Dar es salaam
kuanzia tarehe 25 hadi 26 Machi 2020. Tukio hili muhimu kwa kuwa litakutanisha
watunga sera, watendaji na wanasayansi ambao watatoa taarifa za utafiti kuhusu
hali ya Mabadiliko ya Tabianchi,” alisema.
Alisema Tanzania
inahitaji kuchukua hatua za haraka kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kama
ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika. “Hatua hizo za haraka zinapaswa kuchukuliwa
kutokana na hali halisi iliyopo na inayoendelea ya majanga kama vile mafuriko,
mvua zisizotabirika, ukame na kukosa mazao.
Pia vifo vya wanyama,
kuongezeka kwa kina cha bahari, majichumvi katika maji baridi, na magonjwa yanayoambatana
na Mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza.
Mkurugenzi huyo alisema
athari za Mabadiliko ya Tabianchi zimekuwa hatarishi zaidi kwa watu; zinaathiri
sekta zote za maendeleo, kupunguza/kudumaza jitihada za kufikia maendeleo na
mafanikio.
“Mkutano utakuwa na
tija katika kuhamasisha uwajibikaji wa masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na
kujenga mahusiano stahiki ili kuharakisha jitihada za kukabiliana na Mabadiliko
ya Tabianchi.
Pia kusaidia kuiweka
Tanzania katika uelekeo wa kupunguza utegemezi wa malighafi zinazopelekea
uzalishwaji wa hewa ukaa na kustahimili athari za Mabadiliko ya Tabianchi
zisizoepukika,” alisema.
Damas alisema mwaka
huu, mkutano utakuwa na kauli mbiu: Sayansi, Sera na Utekelezaji: Ushiriki wa
Pamoja Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, Uelekeo Stahiki Kupunguza
Hewa Ukaa na Maendeleo Endelevu.
Kwa upande wake Meneja
Miradi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Kuendeleza Nishati
Tanzania (TaTEDO), Mary Swai alisema athari za Mabadiliko ya Tabianchi ni kubwa
hivyo jamii inapaswa kubadulika na kutumia mbinu mbadala.
Swai alisema TaTEDO
imekuwa ikifanya kazi na jamii hasa yenye kipato cha chini ili kuwezesha
kuondokana na nishati ambazo zinahatarisha madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi.
“Sisi tumekuwa
tukisaidia jamii kutumia vyanzo mbadala katika shughuli zinazohitaji nishati
msingi mkubwa ni kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi na kusema ukweli
kuna hatua kidogo ni imani yetu kongamano hilo litaweza kutoa hali halisi,”
alisema.
Meneja huyo amesisitiza
matumizi ya vyanzo mbadala ambavyo haviathiri mazingira ili kuhakikisha madhara
kama ya joto, ukame na magonjwa yanaepukika.
Naye Mratibu wa Kampeni
kutoka OXFAM, Mkamiti Mgawe alisema mabadiliko hayo yameathiri jamii hasa
wakina mama ambao wanajihusisha na kilimo kutokana na kukosekana kwa utabiri
sahihi wa mvua na kuibuka wadudu haribifu.
“Mabadiliko ya
Tabianchi yamebadilisha sana sekta mbalimbali hasa kilimo ambacho kinahusisha
kundi kubwa la Watanzania,” alisema.
Mgawe alisema wakati
umefika kwa kuwepo sera nzuri ambazo zitaweza kumnufaisha kila mdau ambayo
anataka kuendelea kuishi kwenye ulimwengu hasa mwanamke.
Mtaribu huyo alisema
dunia nzima inapambana kuhakikisha kiwango cha joto cha 1.5 hakifikiwi na njia
ya kufanikiwa katika hilo ni kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Tunaposema Mabadiliko
ya Tabianchi sio jambo dogo kwani yanasabaisha magonjwa, ukame, njaa, joto,
uharibifu wa miundombinu, wadudu na mengine mengi ni jambo pana linahitaji
ushiriki wa kila mdau,” alisema.
No comments:
Post a Comment