Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia) na Mkuu wa Gereza Kwitanga,
Mrakibu Mwandamizi, Dominick Kazmil wakiangalia matunda ya mchikichi
yaliyovunwa katika gereza hilo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kutaka Gereza la
Kwitanga lililopo wilayani Kigoma kuwa
Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa
kufufua kilimo cha zao hilo. Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (watatu mstari wa mbele) akimsikiliza Mkuu wa Gereza Kwitanga, Mrakibu Mwandamizi, Dominick Kazmil
baada ya kuangalia miche ya michikichi iliyooteshwa katika gereza hilo ikiwa ni utekelezaji wa
agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka
Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa
kufufua kilimo cha zao hilo.Wengine ni ujumbe uliofuatana na Naibu Waziri.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Matunda ya Mchikichi
yaliyovunwa katika mashamba ya Gereza Kitwanga yakiwa yameanikwa juani tayari
kwa kukamuliwa mafuta ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kutaka Gereza hilo lililopo wilayani Kigoma kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa
kufufua kilimo cha zao hilo.Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi
Wetu, Kigoma
Wafungwa 150 kutoka
katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa katika Gereza la
Kwitanga Mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa Serikali kuliteua gereza
hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la mchikichi nchini.
Hayo yamesemwa leo na
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara
ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa maagizo na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya ziara gerezani hapo ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza
kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.
“Katika kutekeleza
agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la serikali, wizara
tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na muda si mrefu tutaongeza
wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza
uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari 6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba
na kusambaza mbegu zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi
za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” alisema Masauni
“Lakini pia ili
kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la
Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika kundi la magereza
yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa matatizo yao ya kifedha badala
ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini ambayo inakua haitoshi.
Akizungumza katika
ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri aliunga
mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali huku
akikiri baadhi ya masuala kukwama kutokana na changamoto za kibajeti.
“Nafikiri hili suala la
gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali litatatua changamoto nyingi za
kibajeti na kiuendeshaji maana gereza halina gari kubwa kwa ajili ya uvunajina
usafirishaji wa mafuta kutoka gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya
uendeshaji kwa mfano kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita
1000 hivyo fedha kwa ajili ya kununulia umeme ili kusukuma maji ni changamoto, kwahiyo
kuingizwa kwenye shirika itasaidia changamoto nyingi” alisema ACP Bushiri
Sambamba na kulima zao
la mchikichi Gereza Kwitanga linalima pia mahindi, mpunga, mihogo, maharage na
Bustani za mbogamboga.
No comments:
Post a Comment