HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 05, 2020

WANANCHI WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MFUKO WA BIMA YA AFYA YA JAMII

 Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Temeke wakipima afya wakati wa hitimisho la Wiki ya Madaktari kwa mwaka 2020, iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Mtandao wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA). Upimaji huo ulifanyika katika viwanja vya Zakhem Mbagala, Dar es Salaam.
  Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Tamisemi, anayeshughulikia afya, Josephat Kandege, amewahimiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kama wana maradhi akiwataka pia kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wanapougua.

Kandege ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha wiki ya Madaktari nchini, iliyokwenda sanjari na upimaji afya kwa wananchi, zoezi lililoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kushirikiana na Mtandao wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) na wadau wengine kwenye viwanja vya Zakhem Mbagala.

“Kuna umuhimu kwa kila mmoja kupima afya kwani sasa magonjwa yasiyoambukiza na kuongoza kwa kusababisha vifo. Gharama za kutibu hatua za awali za magonjwa yasiyoambukiza ni ndogo kuliko baada ya ugonjwa kukua. 
Hapa nawashukuru Madaktari na wote walioshirikiana kufanikisha zoezi hili. Mimi leo pia nimepima, ninajua afya yangu…,” alisema Kandege na kuongeza:

“Lakini pia niwaombe kila mwananchi wa Dar es Salaam ajiunge na CHF ili kuwa na uhakika wa afya na kupata tiba kwa wakati.”

Awali, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza(TANCDA), Profesa Andrew Swai, alisema magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kutokana na mtindo wa maisha na kuigharimu Serikali kiwango kikubwa cha fedha kuhudumia wagonjwa.

“Wananchi tukipima afya, na kujua afya zetu na kubadili mtindo wa maisha, tutaepuka magonjwa yasiyoambukiza ambayo sasa yanaua watu wengi kuliko yanayoambukiza na Serikali itatumia fedha kidogo katika kuyadhibiti. Tufanye mazoezi, tupime afya, tule chakula bora, kulinda afya zetu,” alisema Profesa Swai.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Elisha Osati alisema chama chao kina kanda tisa na kwamba zoezi kama hilo limefanyika pia katika katika kanda nane zilizosalia.

Alisema MAT ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali na Serikali kuendeza zoezi la upimaji afya kwa wanachi ili kuisadia Serikali kuboresha afya za wananchi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Gwamaka Mwabulambo aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, aliishukuru MAT kwa kuwajali wananchi wa Temeke ambapo alieleza kwa manispaa hiyo sasa zoezi la upimaji afya kwa wananchi ni endelevu, akiwahimiza wananchi kujali afya zao.

“Aprili 13 tutakuwa na mkesha wa mbio za Mwenge, kwa kushirikiana na MAT kufanya zoezi hili, hivyo wananchi tujali afya zetu.” alisema Dk. Gwamaka. 

Katika hafla hiyo MAT ikishirikiana na wadau mbalimbali, wananchi zaidi ya 500 walipima afya zao kujua kama wana magojwa yasiyoambukiza na Ukimwi.

No comments:

Post a Comment

Pages